Na. Lina Sanga - Kahama
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Makambako leo limefanya ziara ya Kikazi,katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama yenye lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya Uendeshaji wa Halmashauri ikiwa ni pamoja na ukusanyaji Mapato,uwekezaji na ukuzaji wa wananchi kiuchumi kupitia mapato ya ndani na Mikopo ya asilimia 10 iliyokuwa ikitolewa kwa vikundi vya Vijana,Wanawake na watu Wenye Ulemavu.
Katika ziara hiyo Wahe. Madiwani pamoja na baadhi ya wakuu wa idara na vitengo,wamepata fursa ya kutembelea eneo la uwekezaji wa viwanda la Ummy Mwalimu lenye ukubwa wa ekari 500,ambalo limetengwa kwa ajili ya viwanda vidogovidogo kwa mtu mmoja mmoja na vikundi.
Katika eneo la Ummy Mwalimu kuna baadhi ya vijana ambao ni wanufaika wa mikopo ya asilimia 10,ambao kwa sasa wanamiliki viwanda vidogo vya kutengeneza samani za ndani na kuzalisha ajira kwa vijana wengine ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwawezesha vijana kiuchumi na wananchi kwa ujumla.
"Tulitenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo kwa kutoa maeneo bure kwa vijana wanaojitambua na fedha walizonazo kutumia kufanya uwekezaji,Halmashauri tulitoa hati ya kiwanja ambayo mnufaika aliweza kwenda benki na saccos kupata mkopo na kufanya uwekezaji,Halmashauri tunakusanya mapato,kodi na ushuru wa huduma baada ya kuwawezesha wananchi wetu kiuchumi na kuhakikisha tunanunua bidhaa zao ili wakue kutoka nafasi moja hadi nyingine na tumefanikiwa pakubwa"alisema Anderson Msumba, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.
Kupitia ziara hiyo Wahe. Madiwani pamoja na Wakuu wa idara na vitengo wamepata nafasi ya kutembelea maeneo ya uwekezaji uliofanywa na vijana katika eneo la Ummy Mwalimu na stendi ndogo ya mabasi ambayo imesheheni vibanda vilivyojengwa na wajasiriamali wadogo ambao walikuwa maeneo yasiyo rasmi na kwa sasa wamepata eneo rasmi kwa ajiri ya biashara na wanapata mikopo kupitia benki na saccos kwa urahisi na kulipa mapato ya Serikali baada ya kuwezeshwa kiuchumi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa