Na. Lina Sanga
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Makambako limeridhia pendekezo la kuweka mkakati maalumu wa Halmashauri ya Mji Makambako la kutwaa maeneo makubwa pembezoni mwa Mji ili yatumike kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa shule na miradi mikubwa ya uwekezaji pamoja na uanzishwaji kwa Shule maalumu ya vipaji ya wanafunzi wa kike na shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita ili kupunguza adha ya wanafunzi kukosa nafasi ya kuendelea na masomo baada ya kufaulu kidato cha nne.
Akiwasilisha pendekezo la Halmashauri kutwaa maeneo katika Mkutano wa baraza la Madiwani lililofanyika leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Mji na Mazingira, Mhe. Alimwimike Sahwi amesema kuwa kamati hiyo imetoa pendekezo hilo ili kupunguza changamoto ya uhaba wa fedha kwa ajili ya kulipa fidia badala yake,Halmashauri itwae maeneo ya watu na kuyapima na kugawana viwanja kwa utaratibu wa viwanja,asilimia 60 kwa mwenye eneo na asilimia 40 kwa Halmashauri kama gharama ya kufidia upimaji.
Mhe. Sahwi amesema kuwa,kwa utaratibu huo Halmashauri itaweza kuwa na miradi ya viwanja ambavyo inaweza kuuza na kupata fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kupata maeneo ya huduma za jamii kama vile ujenzi wa shule, masoko na vituo vya afya.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi,afya na elimu,Mhe. Imani fute amewasilisha pendekezo la kamati hiyo la kuanzishwa kwa shule ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Maguvani na shule ya vipaji maalumu ya wanafunzi wa kike wenye ufaulu mkubwa katika shule ya sekondari Mlowa kuanzia mwezi januari,2023 kwani shule hizo zina miundombinu inayowezesha uanzishwaji wa shule hizo.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa