Na. Lina Sanga
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji Makambako leo limeiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutengua kauli ya kuwaruhusu wafanyabiashara wa mazao kufanyia biashara nje ya soko mahususi kwa biashara hiyo,ili kufuta hoja ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kuhusu utekelezaji wa mradi wa soko hilo.
Wajumbe wa baraza wametoa ombi hilo katika mkutano maalum wa baraza la madiwani la kupitia hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 uliofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Makambako.
Wajumbe wamesema kuwa, kutokana na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka kuruhusu wafanyabiashara kufanya biashara nje ya soko la mazao Kiumba,huenda limetokana na kutokuwa na taarifa sahihi kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wachache ambao wanakinzana na maamuzi ya baraza la Madiwani na Mpango wa Halmashauri wa kupanga Mji.
Baraza hilo limeiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe kupitia upya utekelezaji wa mradi wa soko hilo kwani Halmashauri imewekeza zaidi ya Mil. 300 na wananchi wamekopa ili kujenga maghala na vizimba, kutokutumika kwa soko hilo kumedhoofisha uchumi wa wananchi na Serikali inakosa mapato lakini pia maeneo mengine yameathiriwa kama ukusanyaji wa ushuru wa vibanda kutokana na agizo hilos.
Bw. Willy Undule, mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali Mkoani Njombe ameungana na Madiwani kuiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe kushughulikia suala la soko la mazao Kiumba kwa busara ili hoja ifungwe, kwani operesheni za Mji wa Makambako zinategemea ukusanyaji wa ushuru kwenye sehemu za biashara hivyo kuua sehemu hizo Mapato ya Makambako yatazidi kushuka.
Bi. Judica Omari , Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe amesema amepokea maoni na maombi ya baraza la Madiwani na kuahidi kulifanyia kazi ili hoja ya soko hilo na maeneo mengine ifutwe.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa