Na. Lina Sanga
Mkuu wa shule ya sekondari makambako, Mwl. Godfrey Fwilla amewataka wanafunzi wa kidato cha nne 2025 kuwa watulivu wenye kusoma maswali yote na kuchagua maswali wanayoyaweza kabla ya kujibu ili waweze kupata daraja linalostahili pamoja na kuzingatia sheria za baraza la mitihani.
Mwl. Fwilla ametoa wito huo leo wakati akizungumza na watahiniwa wa mitihani ya kidato cha nne ambayo inaanza rasmi siku ya jumatatu Novemba 17 hadi Desemba 5,2025.
Ameongeza kuwa, shule ya sekondari Makambako ni shule kongwe katika Halmashauri ya Mji Makambako, hivyo ni matarajio ya wengi kuona shule hiyo inapata daraja la kwanza hadi la tatu kwani kupata ziro ni aibu.
Amewasisitiza watahiniwa hao kutuliza akili wakati wa kuchagua maswali kwa kuyasoma kwa umakini ili waweze kupata daraja linalostahili,kwani cheti cha kidato cha nne ni muhimu sana na ni cheti cha mwanzo kitakachowawezesha kwenda ngazi mbalimbali.
Naye Mwalimu wa taaluma Mwl. Jisena Daudi amekiri kulidhishwa na maandalizi ambayo walimu wamefanya kuhakikisha wanafunzi hao wanapata ufaulu mzuri utaowawezesha kuendelea na elimu ya kidato cha tano na kwenda vyuo mbalimbali.
Kefa Lulandala na Silivya Kahonga, kwa niaba ya wanafunzi wengine ambao ni watahiniwa wa mitihani ya kidato cha nne 2025 wamewashukuru walimu kwa kuwafundisha vizuri na kuwahamasisha hali inayowafanya kujiamini na kukumbushana kumuomba Mungu ili waweze kufanya mitihani yao salama na kupata ufaulu mzuri.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa