Na. Lina Sanga
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Makambako limeishauri Menejimenti kuendesha miradi ya uwekezaji kwa faida ili kuanzisha miradi mipya ya uwekezaji na kuongeza mapato ,badala ya kukopa kwa ajili ya kuanzisha miradi mipya ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mzani katika soko la mazao lililopo Mtaa wa Makatani,Kata ya Lyamkena.
Ushauri huo umetolewa leo katika mkutano wa baraza la Madiwani katika kipindi cha kuishia robo ya kwanza (julai – septemba)katika mwaka wa fedha 2023/2024,uliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri.
Wakitoa ushauri huo kwa nyakati tofauti wajumbe wa baraza hilo wamesema kuwa, ombi la kukopa fedha kwa ajili kuingizwa kwenye biashara ya mzani ambao Halmashauri haijawai kuifanya halikubaliki,hivyo ni vema mradi huo ubinafsishwe au kujengwa kwa mfumo wa jenga,tumia rejesha ili kutoa fursa kwa watu binafsi kuwekeza na Halmashauri kupata asilimia kadhaa.
Aidha, wameipongeza timu ya menejimenti kwa kubuni miradi kwa ajili ya kuongeza vyanzo vya mapato na kuishauri kujikita katika kusimamia miradi iliyopo ,ili fedha zinazozalishwa zitumike kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma na kuanzisha miradi mipya ya uwekezaji.
Mhe. Hanana Mfikwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako amesema kuwa,jambo la Halmashauri kujitegemea na kubuni miradi ni jambo la msingi na Halmashauri inahitaji kuanzisha vyanzo vya mapato , ambavyo vitasaidia kupunguza adha ya kufukuzana na wananchi kwenye kodi mbalimbali , hivyo ni vema vyanzo vilivyopo makusanyo yake yatumike kununua mzani au kuingia ubia na mzabuni au mwananchi anayeweza kuweka mzani kwa mfumo wa jenga,tumia rejesha na sio kubinafsisha.
Amesema kuwa kubinafsisha kwa mtu binafsi kuweka mzani katika soko hilo haiwezekani ,kwani mwisho wa safari Halmashauri itakosa vyanzo vya mapato na kushindwa kubuni vyanzo vingine ,kwani vyanzo vyote vya mapato vitakuwa mikononi mwa wananchi na kuanza kukimbizana na wananchi kuhusu kodi.
Ameongeza kuwa,kwa sasa mambo yanayotakiwa kufanyika ni pamoja na uwekezaji wa Halmashauri, kwa Halmashauri kujipanga kuwekeza kupitia vyanzo vya mapato ambavyo imewekeza,hivyo kujenga kwa mfumo wa jenga,tumia,rejesha inawezekana vinginevyo Halmashauri ijenge mzani fedha zitakapo patikana.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa