Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Njombe (DAS),Emmanuel George wakati wa ufunguzi wa semina ya uhamasishaji wa chanjo ya uviko 19, iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Mji Makambako.
Bw. Emmanuel amesema kuwa serikali imeamua kuhamasisha watu kupata chanjo kutokana na dhana potofu kwa baadhi ya watu juu ya chanjo ya uviko 19 ambayo imepokelewa kwa mitazamo tofauti na chanjo zingine zilizowahi kutolewa kama chanjo ya tetenasi,surua na homa ya ini.
“Kila mtu atambue kuwa jukumu la kuhamasisha wengine kupata chanjo ya uviko 19 ili kupunguza kasi ya maambukizi na kupunguza idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huu,kwani ambao walishapata maambukizi na kupona wanajua maumivu ya ugonjwa huu,hivyo uhamasishaji uanzie katika ngazi ya kaya zetu na jamii kwa ujumla kwa kila mmoja kutambua umuhimu wa kujilinda na kuwalinda wengine” alisema Bw. Emmanuel.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Makambako, Dtk. Alexander Mchome amesema kuwa katika halmashauri ya Mji Makambako wananchi waliopata chanjo ya uviko 19 ni 687 sawa na asilimia 16.3 ya dozi lengwa 4220 ya J&J.
Dkt. Mchome amebainisha kuwa watu wengi ambao bado hawajapata chanjo wanajificha kwenye kauli iliyowahi kutolewa na Hayati John Pombe Magufuli aliyekuwa raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliposema kuwa tusiharakishe kupokea chanjo hadi tujiridhishe kama ni salama kwa watanzania,na kwa sasa wataalamu wamejiridhisha kuwa ni salama ndio maana wananchi wanahamasishwa kuchanja.
Akitolea ufafanuzi wa suala la kuganda kwa damu kama ambavyo watu wengine wanavyohofia,Dkt Mchome amesema kuwa wapo baadhi ya watu wanakabiliwa na tatizo la kuganda kwa damu hata kabla ya kupata chanjo,hivyo watu wajitokeze kupata chanjo hiyo kwani wataalamu wameshajiridhisha kuwa haina madhara kwa watu.
Akitolea ufafanuzi wa uzushi unaosambazwa mitaani juu ya chanjo hiyo, Mratibu wa huduma za chanjo katika halmashauri ya Mji Makambako,Tindichebwa Mazala Amesema kuwa sio kweli kwamba mtu aliyepata chanjo atageuka kuwa zombie kama watu wengine wanavyosema,wala hakuna sumaku kwenye mwili wa mtu aliyepata chanjo na chanjo hiyo haibadilishi vinasaba vya mtu wala kusababisha matatizo ya uzazi kama ugumba na upungufu wa nguvu za kiume,watu wajitokeze kupata chanjo ili kujilinda wao wenyewe na wanaowazunguka.
Semina hiyo iliwashirikisha madiwani,watumishi wa umma,viongozi wa dini na serikali,Viongozi wa wafanyabiashara,viongozi wa bodaboda na bajaji.
#TOKOMEZA UVIKO 19
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa