Na. Lina Sanga
Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa amewataka wananchi katika Kata ambazo zimepokea fedha,kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya kidato cha kwanza 2023,kushiriki ujenzi wa madarasa hayo ili fedha zilizotolewa na Serikali Kuu zitoshe kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa.
Mhe. Kissa ametoa agizo hilo jana katika ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi hiyo,katika Halmashauri ya Mji Makambako na kuwaagiza Wenyeviti wa Mitaa,kuwashirikisha wananchi katika utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha kila mwananchi wa eneo husika anafanya kazi mbalimbali katika eneo la ujenzi kama kusafisha eneo,kuchimba msingi,kusogeza tofali na kazi zingine.
“Ndugu zangu fedha zilizotolewa kwa ujenzi wa madarasa hazitaweza kukamilisha ujenzi wa madarasa,endapo kazi zote ataachiwa fundi,hivyo Wenyeviti wote wa Mitaa ambayo kuna ujenzi wa madarasa hakikisheni mnawashirikisha wananchi hatua zote za utekelezaji wa miradi hii,kuanza taarifa za mapokezi za fedha na kufanya kazi mbalimbali za ujenzi ili fedha zilizoletwa na Serikali Kuu zikamilishe ujenzi wa madarasa tofauti na hapo hatutafanikiwa”,alisema Mhe. Kissa.
Aidha,amewataka wananchi kuimiliki miradi na kuisimamia kwani ni miradi yao na wana haki ya kujua kila hatua ya ujenzi wa miradi hiyo,hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki ili aweze kuulinda mradi na kuwa na uchungu nao.
Nao Madiwani wa Kata zilizopokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa hayo,kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa fedha za ujenzi zilizotolewa,kwani zitasaidia kuwapunguzia wananchi mzigo wa michango na kuahidi kushirikiana na wananchi wao bega kwa bega ili ujenzi wa madarasa hayo ukamilike ndani ya muda uliopangawa.
Halmashauri ya Mji Makambako imepokea jumla ya shilingi Mil. 420 za ujenzi wa madarasa ishirini na moja kwenye shule sita,ambazo ni Makambako Sekondari madarasa 6,Mlumbe Sekondari madarasa 3,Deosanga Sekondari madarasa 4,Maguvani Sekondari madarasa 3,Kitandililo Sekondari madarasa 2 na Mahongole Sekondari madarasa 3 kila darasa moja linagharimu shilingi Mil. 20 pamoja na Madawati.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa