Na. Lina Sanga
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika Halmashauri ya Mji Makambako tarehe 8 machi,katika Uwanja wa Polisi Mjini hapa.
Mhe, Kissa alisema kuwa kiuchumi wanawake wana mchango Mkubwa sana,mwanamke ukimpa fedha anakuletea utajiri,lakini kumekuwa na tabia ya wanawake wengine kutofurahia mafanikio ya wengine.na kuweka vikwazo ili kuwakwamisha wanawake wenzao wanapopata mafanikio katika kazi, kwa kukanyaga magauni huku wakiwashangilia ili waendelee kupiga hatua waanguke katika nafasi zao.
“Wanawake wenzangu tuache kukanyaga magauni ya wenzetu ili kuwakwamisha bali tuinuane ili kufikia mafanikio,mwenzako anapopiga hatua ya mafanikio mpongeze na kumuunga mkono,kama hapa kuna wanawake wanauza matunda kila mwanamke anunue matunda kuunga mkono juhudi za wanawake wenzetu wajasiriamali”,alisema Mhe. Kissa.
Katika ngazi ya jamii,Mhe. Kissa alisema kuwa Mwanamke amekuwa nguzo bora katika Malezi kuanzia ngazi ya familia,kwa kuhakikisha familia yake ipo vizuri na kuwafundisha watoto malezi bora lakini pia kuhakikisha usalama wa familia na jamii pamoja na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Siasa alisema kuwa,Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefungua kamba na kuvunja mwiko ambao ulikuwa kama fimbo ya kuwachapia wanawake na kuwapa vitisho,juu ya kushika nafasi za juu katika ngazi ya Utawala na Uongozi.
“Mama Samia amefungua kamba na amevunja mwiko kwamba hapa kote piteni lakini pale msipite maana msitu ule una nyoka wanene mwanamke ukifika utaliwa na nyoka,leo Mama Samia amevunja mwiko,kina mama tumuunge mkono Rais wetu,watu wengine wanaweza wakahoji kwanini mwanamke mwenzetu,naomba niwaambie wanawake wenzangu tusipotumia hii fursa hatutapata nafasi nyingine tena ya sisi kuingia katika nafasi hiyo”,alisema Mhe. Kissa.
Sambamba na Maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa alimkatia bima ya afya mtoto mwenye ulemavu wa viungo na kuwatua masinia ya matunda wanawake wajasiriamali,waliofika kwenye Maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani kwa kununua matunda yote kwa kushirikiana na wakuu wa idara wanawake katika halmashauri ya Mji Makambako,Waheshimiwa Madiwani pamoja na taasisi mbalimbali zilizofika katika Viwanja hivyo.
Mwisho.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa