Na. Lina Sanga
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda ameitaka Halmashauri ya Mji Makambako kuhakikisha bajeti mpya ya mwaka 2025/2026,inazingatia vipaumbele vilivyopo kwenye Kata hususani miradi viporo, ili kupunguza maswali kwa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu.
Mhe. Sweda ametoa wito huo leo katika Mkutano wa baraza la Madiwani kwa Kipindi cha kuishia robo ya pili, kwa mwaka wa fedha 2024/2025 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Ameongeza kuwa, Makambako ni lango la Mkoa na ni Mji wa kibiashara hivyo, idara ya ardhi haina budi kuisaidia Halmashauri kupata maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda, ili kuongeza mapato ya Halmashauri na kuwawezesha wananchi kufanya uwekezaji, kwani usafirishaji wa bidhaa ni rahisi kwa usafiri wa barabara au reli.
“Maono ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe ni kuibadilisha Makambako kuwa sehemu nyingine kabisa ya uwekezaji, Makambako imechangamka na baada ya muda mfupi itabadilika na mtakuwa mnapata mapato na kuachana kukimbizana na wakulima wa nyanya wenye robo eka kukusanya ushuru,kwa sababu kuna viwanda na unakusanya kodi ya huduma ya kutosha,nina omba sana mfanye maamuzi sahihi kwa ajili ya viwanda”,alisema Mhe. Sweda.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako, Mhe. Salum Mlumbe kwa niaba ya baraza la Madiwani na watumishi amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda kuufanyia kazi ushauri aliotoa na kumkaribisha kuwatembelea kwenye Kata ili aweze kuijua Wilaya na watu anaowaongoza.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa