Na. Lina Sanga
Familia na jamii zimeelezwa kuwa ni kikwazo cha wana ndoa wengi kuendelea na kesi za unyanyasaji wa kijinsia,na matukio ya ukatili unaofanyika ndani ya familia dhidi ya wanawake na watoto pindi zinapofikishwa Mahakamani kwa kuhofia kutengwa.
Hayo yamebainishwa na James Maroda,Hakimu Mkazi katika Mahakama ya Mwanzo Makambako,katika kikao cha MTAKUWA kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Makambako kwa ajili ya kupokea mrejesho wa shughuli za uelimishaji masuala ya ukatili na afya ya uzazi,zilizofanyika agosti 16,mwaka huu kupitia ushirikiano wa shirika la JEUMA na hospitali ya Marie Stopes Makambako.
Maroda amesema kuwa,wanawake wengi baada ya jalada la kesi yake kufikishwa mahakamani,kabla ya shitaka kusikilizwa husitisha kusikilizwa kwa shitaka hilo kwa madai ya kukaa vikao vya usuluhisho vya familia,lengo la mahakama ni kuleta amani na sio kuwachonganisha.
“Mwanamke anapokuja mahakamani yupo pamoja na wana familia,Unapomsomea shitaka mama ananyoosha mkono na kusema mheshimiwa hakimu nimemsamehe mume wangu,unamuuliza kusudio la kuleta kesi mahakamni ni nini?,anasema wameshakaa na ndugu pande za mume na mke na wamesuluhishwa hivyo endapo hakimu akiendeleza kesi watasema Mahakam ndiyo imeamua,kwa kuwa uwepo wa mahakama ni amani katika jamii na sio kuifitinisha jamii”,alisema Maroda.
Naye,Afande Happy Edward kutoka ofisi ya dawati linaloshughulikia masuala ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kutoka kituo cha polisi Makambako,amesema kuwa kitendo cha wanawake kuwa wepesi wa kusamehe kabla ya kusikilizwa kwa mashitaka yanayofikishwa mahakamani,ni chanzo kikubwa cha ongezeko la matukio hayo kwani hadi sasa jumla ya matukio ya unyanyasaji na ukatili wa wanawake na watoto yaliyoripotiwa yamefikia asilimia 85.
Lakini pia kutokana na malalamiko ya wanaume kushindwa kuripoti unyanyasaji wa kijinsia kwa madai ya kukosekana kwa Maaskari wa jinsia ya kiume katika ofisi ya dawati,Afande Manyumba Edward kutoka ofisi ya dawati katika kituo cha polisi Makambako ametoa wito kwa wanume kujitokeza kwani kwa sasa ofisi hiyo kuna maaskari wa kiume wapo kwa ajili ya kuwasikiliza na kuwasaidia kupata haki zao na kuwataka kutokutumia nafasi hiyo kutekeleza matukio ya kikatili kwa wengine.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa