Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako imepongezwa kwa kuvuka vizuri hatua ya ukaguzi wa hesabu za Serikali na kupata hati safi mfululizo tangu kuanzishwa kwa Halmashauri mwaka 2012.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe,Bi. Judica Omari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka katika mkutano maalum wa baraza la madiwani la kupitia mpango kazi na majibu ya menejimenti kwa ajili ya utekelezaji wa hoja za mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali kuishia juni 30,2022.
Judica amesema kuwa,kupata hati safi mfululizo ni kiashiria kikubwa cha uwepo wa ushirikiano baina ya Madiwani na wataalamu katika kusimamia miongozo,sheria na kanuni katika usimamizi fedha zilizopo kwenye bajeti na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo imepokea fedha nyingi kutoka Serikali kuu na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Aidha,ameipongeza Halmashauri ya Mji Makambako kwa kufikia asilimia 95 ya ukusanyaji wa mapato na kutoa rai kwa Menejimenti kuhakikisha asilimia 5 iliyobaki inapatikana na kufikia asilimia 100 ya ukusanyaji wa mapato ifikapo juni 30,mwaka huu.
Naye,Willy Undule, Mkaguzi Mkuu wa hesabu Mkoa wa Njombe, amepongeza na kutoa rai kwa Halmashauri ya Mji Makambako kuendeleza ushirikiano katika utendaji kazi ili kuendelea kupata hati safi na kuhakikisha hoja zilizobaki zinafungwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya kupitia mpango kazi na majibu ya menejimenti kwa ajili ya utekelezaji wa hoja za Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako,Kenneth Haule amesema kuwa,katika taarifa ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka 2021/2022 Halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 20,kati ya hizo hoja 15 zilijibiwa na kufungwa na hoja 5 zilizobaki utekelezaji umefanyika kwa sehemu na ufuatiliaji unaendelea kufanyika.
Pia, katika taarifa ya hesabu za mradi wa mfuko wa Afya wa pamoja kwa mwaka 2021/2022,Halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 4,kati ya hizo hoja 3 zimejibiwa na kufungwa na hoja 1 iliyobaki utekelezaji wake umefanyika kwa sehemu.
Aidha,katika taarifa ya hesabu za mradi wa mfuko wa wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka 2021/2022,Halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 5,kati ya hizo hoja 3 zimejibiwa na kufungwa na hoja 2 utekelezaji wake umefanyika kwa sehemu.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa