Na. Lina Sanga
Mikataba ya lishe itakayotumika kwa miaka nane,imesainiwa leo katika Halmashauri ya Mji Makambako na Mkurugenzi pamoja na Watendaji wa Kata 12 zilizopo katika Mji wa Makambako.
Kabla ya Utiaji saini wa Mikataba hiyo,Mada zinazohusu lishe ziliwasilishwa na Katibu wa Afya wa Halmashauri ya Mji Makambako,Benedict Musiba sambamba na Afisa Lishe Meckfrida Mmari ili kuwajengea uelewa Watendaji juu ya majukumu yao katika usimamizi wa Lishe kwenye Kata zao ili kufanikisha uboreshaji wa lishe kwa watoto chini ya miaka mitano.
Mkoa wa Njombe unakabiliwa na tatizo la Udumavu kwa asilimia 53.6, hali inayoelezwa kuchangiwa na lishe duni kwa watoto chini ya miaka mitano ambapo Halmashauri ya Mji Makambako asilimia 0.9 ya watoto wana tatizo la udumavu na asilimia 0.7 wanakabiliwa na tatizo la ukondefu, unaosababishwa na ukosefu wa virutubisho muhimu katika chakula.
Ili kukabiliana na tatizo la udumavu na ukondefu kwa watoto chini ya miaka mitano,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako,Kenneth Haule ametoa agizo kwa Afisa lishe na Maafisa elimu Msingi na Sekondari kuhakikisha kila shule inakuwa na vitalu vya mbogamboga na matunda badala ya maua,ili zitumike katika vyakula vya wanafunzi shuleni.
Pia,amemuagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Makambako,Dkt. Ally Senga kuhakikisha Watendaji wa Kata,Mitaa na Vijiji wanashirikiana na Kamati za Afya katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali yanayohusu afya na lishe katika Mitaa na vijiji ili kuwajengea uwezo Watendaji wa kutoa elimu ya lishe kwa wananchi.
Aidha,Halmashauri ya Mji Makambako imetenga zaidi ya Mil. 26 kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 ambapo mapato ya ndani ni Mil. 18 ikiwa ni fedha kwa ajili ya lishe ya watoto shuleni, ambapo kila mtoto anatengewa wastani wa shilingi 1,000 ikiwa ni agizo la Serikali.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa