Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako kupitia idara ya Utumishi na Utawala imepokea tuzo ya Utendaji bora kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na kushika nafasi ya kwanza kati ya halmashauri zote za Miji Tanzania .
Tuzo hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora,Mh. Jenister Mhagama (MB) kwa halmashauri zilizofanya vizuri katika utendaji bora,katika kikao kazi kilichoitishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kilichofanyika Jijini Dodoma Mei,2022.
Tuzo hiyo imewasilishwa leo na Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Makambako, Bw. Kenneth Haule katika kikao maalumu cha Kamati ya Fedha na Uongozi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa halmashauri amesema kuwa,tuzo hiyo imetolewa kwa halmashauri ya Mji Makambako baada ya kukidhi vigezo katika utekelezaji wa maagizo ya Serikali kwa wakati na kwa kufuata miongozo inayotolewa.
“Kutokuwa na malalamiko mengi yanayohusu masuala ya watumishi,kuwa na taarifa safi za watumishi,utoaji wa huduma bora kwa wakati na uzingatiaji wa maadili katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya kiutumishi ni vigezo vikuu ambavyo vimeiwezesha halmashauri yetu kushika nafasi ya kwanza kati ya halmashauri zote za Mji Nchini”, alisema Haule.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Makambako ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uongozi, Mhe. Hanana Mfikwa kwa niaba ya madiwani wote, amempongeza Mkurugenzi na timu ya Menejimenti,idara ya Utumishi na Utawala kwa utendaji bora wa majukumu mbalimbali na kufuata miongozo inayotolewa na Serikali na halmashauri ya Mji Makambako kuibuka mshindi kwa kushika nafasi ya kwanza ya Utendaji bora na kunyakua tuzo.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa