Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako kupitia mapato ya ndani,imenunua mashine ya kupima udongo yenye thamani ya shilingi Mil.8.5, ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa tija na kuongeza kipato cha mkulima,kupunguza gharama za uzalishaji na kuboresha utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima.
Akitoa taarifa hiyo kwa kamati ya fedha na uongozi juu ya ununuzi wa mashine hiyo,Beatrice Tarimo kaimu mkuu wa idara ya kilimo,umwagiliaji na ushirika wa Halmashauri ya Mji Makambako amesema kuwa,mashine hiyo ina tumia vitendanishi 50 kwa ajili ya kupima sampuli 50 za udongo.
Tarimo amesema kuwa mashine hiyo ina uwezo wa kupima vigezo kumi ikiwa ni pamoja na nitrogen, phosphorus, potassium, sulphur, manganese, magnesium, calcium,aluminium pamoja na kupima uchachu wa udongo na Uwezo wa udongo kupitisha chaji na mahitaji ya chokaa.
Ili kufanikisha zoezi la upimaji udongo jumla ya maafisa ugani 22 ngazi ya kata na vijiji watapewa mafunzo,juu ya uchukuaji sampuli na kutafsiri matokeo ya maabara kwa wakulima,na mkulima atachangia gharama za upimaji wa udongo kwa kila sampuli moja ambayo itagharimu shilingi 52,000.
Mwenyekiti wa kamati ya fedha na uongozi,Mhe. Hanana Mfikwa pamoja na wajumbe wa kamati ga fedha wamepongeza ununuzi wa mashine hiyo,na kuwaagiza maafisa ugani kuhakikisha huduma ya kupima udongo inafanyika kwa wakati ili wakulima wapate manufaa.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa