Na. Lina Sanga
Mkurugenzi msaidizi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mhandisi Enock Nyanda ameipongeza Halmashauri ya Mji Makambako kwa utekelezaji mzuri wa miradi iliyopata fedha kutoka Serikali kuu.
Nyanda ametoa pongezi hizo katika ziara ya ukaguzi wa miradi iliyopokea fedha kutoka Serikali kuu, iliyofanyika leo katika Halmashauri ya Mji Makambako yenye lengo la kukagua ukamilishaji wa majengo ya madarasa, maabara,zahanati na hospitali na kulinganisha thamani ya fedha iliyotumika katika ukamilishaji wa majengo hayo.
Amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa majengo yote aliyokagua na kutoa rai kwa Mkurugenzi,kuhakikisha majengo yaliyokamilika kuanza kutumika mara baada ya ujenzi kukamilika ili kutoa matokeo chanya kwa wanafunzi na jamii kwa kupata huduma na kunufaiki kupitia majengo hayo.
Kwa upande wa miradi ya ujenzi wa zahanati za vijiji na mitaa,Nyanda amesema kuwa baada ya majengo hayo kukamilika,yaanze kutoa huduma kwa jamii huku ukamilishaji wa miundombinu mingine ikiendelea kujengwa na changamoto ya nyumba za watumishi itafutiwe ufumbuzi na kuwaagiza watendaji wa Kata na Mitaa kwa kushirikiana na wajumbe wa kamati za ujenzi,kuwatafutia watumishi nyumba za kupanga wakati mchakato wa ujenzi wa nyumba za watumishi ukiendelea hasa kwa maeneo ya pembezoni mwa mji.
Kuhusu Madarasa na Maabara,Mhandisi Nyanda ameipongeza Halmashauri ya Mji Makambako kwa kutumia vizuri fedha zilizoletwa kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara na madarasa,kwa kuzingatia mahitaji halisi yaliyopo na kuokoa fedha kwa kiasi kikubwa na kuzitumia kupunguza uhaba wa majengo mengine na huduma muhimu kama miundombinu ya maji shule ya sekondari mukilima,ofisi ya mwalimu mkuu shule ya msingi Ushindi na matundu ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi shule ya sekondari Deosanga na ujenzi wa maabara ya kisasa shule ya sekondari Makambako.
Ametoa wito kwa Mkurugenzi kukutana na menejimenti za shule na kujadiliana kuhusu kuongeza ufaulu wa wanafunzi,kwani Serikali imeshajenga madarasa na maabara jukumu lililobaki ni kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi pekee.
“Serikali inafarijika sana kuona ufaulu mzuri wa wanafunzi ukiongezeka kila mwaka,hivyo ni vema Mkurugenzi kukaa na walimu kujadiliana nao kuhusu mbinu za ujifunzaji na ufundishaji hasa kwa shule ambazo hazifanyi vizuri kwa sasa,ili kutambua changamoto zinazosababisha kupatikana kwa ufaulu hafifu wa baadhi ya wanafunzi lakini pia suala la ujenzi wa hosteli ni vema lianze kufikiriwa ili kuwasaidia wananfunzi kupata muda mwingi wa kujisomea”, alisema Nyanda.
Baadhi ya Miradi iliyopokea fedha kutoka Serikali kuu ni pamoja na ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mahongole mil 50, Zahanati ya Maguvani mil 50, Ukamilishaji wa darasa moja shule ya msingi Manga mil 21.2,Ujenzi wa maabara Maguvani sekondari mil 25.9,Maabara lyamkena sekondari mil 25 na madarasa mawili yenye thamani ya mil 22.5, maabara Makambako sekondari mil 41,Mukilima sekondari maabara yenye thamani ya mil 25,ukamilishaji wa madarasa mawili Deosanga sekondari yenye thamani ya mil 10.4 pamoja na vyoo matundu 11 vyenye thamani ya mil 12.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Kenneth Haule pamoja na watumishi wa Hamashauri ya Mji Makambako wameishukuru Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanazania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa fedha zilizotolewa na kukamilisha maboma ya madarasa, zahanati na maabara kwa ajili ya masomo ya Sayansi,nakuahidi kutoa huduma bora kwa wananchi na kuongeza Ufaulu wa wanafunzi.
#jiandaekuhesabiwa2022
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa