Na. Lina Sanga
Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa ameipongeza Halmashauri ya Mji Makambako kwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa ya kidato cha kwanza 2023 kwa wakati na kwa kuzingatia ubora, na kumuagiza Mkurugenzi kumwandikia barua ya pongezi Mwenyekiti wa Mtaa wa Sigrid kwa kushiriki usimamizi wa ujenzi wa madarasa sita katika shule ya Makambako Sekondari iliyopo katika Mtaa anao uongoza.
Mhe. Kissa ametoa pongezi na agizo hilo leo katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa ya kidato cha kwanza 2023,katika shule sita za Sekondari za Halmashauri ya Mji Makambako.
Amesema kuwa katika miradi yote ya madarasa mwenyekiti wa Mtaa wa Sigrid,Bahati Nyato tangu mwanzo wa utekelezaji wa ujenzi wa madarasa amekuwa bega kwa bega na walimu katika usimamizi wa mradi bila kulazimishwa,kwani hata alipofanya ziara ya kushitukiza alimkuta eneo la mradi.
“Mkurugenzi naomba huyu mwenyekiti wa mtaa aandikiwe barua ya pongezi kwa kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa mradi huu wa ujenzi wa madarasa sita,kwani binafsi nimemkuta Mwenyekiti huyu na Mwalimu katika mradi huu pindi nilipokuja bila taarifa na anaonekana anajali na amejitoa mwenyewe kushiriki bila kulazimisha,hongera sana Mwenyekiti kwa kujitoa”,alisema Mhe. Kissa.
Aidha, Mhe. Kissa amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo,kwani madarasa yamejengwa kwa ubora wa hali ya juu na uhakika wa wanafunzi kuyatumia madarasa hayo januari,2023 upo.
Ametoa agizo kwa Shule zote zenye ujenzi wa madarasa ya kidato cha kwanza kukamilisha madarasa yote ndani ya muda uliopangwa,kabla ya tarehe ya mwisho ya kukabidhi madarasa ngazi ya taifa,kwa kuhakikisha umaliziaji wa baadhi ya vitu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Halmashauri ya Mji Makambako ilipokea jumla ya Mil. 420 za ujenzi wa madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023,ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa michango ya ujenzi wa madarasa.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa