Na. Lina Sanga
Uzinduzi wa kliniki ya ardhi wafanyika leo katika Mtaa wa Ilangamoto,Kata ya Lyamkena kuadhimisha wiki ya huduma kwa mteja kwa kutekeleza shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi kama kugawa hati miliki kwa wananchi,kutatua kero mbalimbali,kupokea maombi ya vibali vya ujenzi sambamba na kuandaa hati miliki kwa maeneo yaliyopimwa.
Akizungumza na wananchi wa Mtaa huo Mthamini Mkuu Msaidizi Wizara ya ardhi, Dkt. Adam Nyaruhuma amewapongeza wananchi waliokabidhiwa hati na kuwataka wazitunze na kuzitumia vizuri kiuchumi na kuwasisitiza nidhamu katika matumizi sahihi ya viwanja vilivyopimwa kwa kutokatakata vipande bila kuwashirikisha wataalamu wa ardhi kwani lengo la upimaji ni pamoja na kupanga mji.
Bi. Flaviana Mamkwe, Msimamizi wa sekta ya ardhi Halmashauri ya Mji Makambako amesema kuwa Mtaa wa Ilangamoto umepangwa na kupimwa ambapo jumla ya michoro 16 ya mipango miji imeandaliwa na viwanja 800 vimepimwa.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kupata huduma za ardhi katika Mtaa wao ambazo zitatolewa kwa siku tano gharama zote zimelipwa na Wizara ya ardhi.
Bw. Geofrey Johson na Thomas Kiwale wakazi wa Mtaa wa Ilangamoto ambao leo wamekabidhiwa hati zao, wametoa rai kwa wananchi wengine kufanya taratibu za kupata hati miliki za viwanja vyao ili kuthibitisha umiliki wao na kutoishi kama wakimbizi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa