Na. Lina Sanga
Jamii imetakiwa kutambua umuhimu wa wauguzi kutokana na majukumu waliyonayo, katika kuhakikisha afya za watu zinaimarika.
Wito huo umetolewa leo na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe,Bi. Judica Omari kwa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani 2023, ambayo katika Mkoa wa Njombe Maadhimisho hayo yamefanyika Halmashauri ya Mji Makambako katika uwanja wa polisi.
Bi. Judica amesema kuwa,wauguzi hukaa na wagonjwa masaa mengi na kumfariji Mgonjwa hadi dakika za mwisho ,hivyo jamii ina kila sababu ya kutambua umuhimu wa wauguzi na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayofanya.
Amesema kuwa,licha ya kazi kubwa wanazofanya wauguzi,wapo baadhi yao sio waadilifu na wanafanya kazi kinyume na maadili ya kazi zao kwa kufanya vitendo visivyokubalika kama kutoa lugha zisizofaa kwa wagonjwa,kupokea rushwa na kutoa taarifa za siri za wagonjwa na kuwataka wauguzi wenye tabia hizo kuacha mara moja kwani vitendo hivyo havikubaliki.
Kuhusu uhaba wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya,amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imeweka utaratibu wa kutoa vibali vya ajira kila mwaka ,na kipaumbele ni sekta ya afya ili kupunguza changamoto ya uhaba wa wauguzi na wakunga kwenye vituo vya afya nchini.
Aidha,ametoa wito kwa Wakurugenzi kuhakikisha wanaandaa mazingira rafiki kwa ajili ya watumishi wanaoajiriwa, ili pindi wanapoajiriwa wabaki Mkoa wa Njombe na kuwa tayari kuwapokea watumishi wote watakaoajiriwa.
Pia,amewaagiza wauguzi wote kusimamia mapato yanayokusanywa kwenye vituo vya afya na kutoka Serikali kuu,kwa kuhakikisha mapato yanapatikana asilimia 50 ya mapato lindwa yanaelekezwa kwenye ununuzi wa dawa na vifaa tiba ili huduma iwe endelevu na asilimia inayobaki inatumika katika huduma mbalimbali kama posho,usafi wa Zahanati na mahitaji mengine.
Mwisho amewasihi wauguzi wote kutekeleza viapo vyao kwa kufanya kazi kwa upendo,kujitoa na kushirikiana ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa