Na. Tanessa Lyimo
Halmashauri ya Mji Makambako kwa kushirikiana na wananchi, imeanza maadhimisho ya siku ya upandaji miti kwa kupanda miti katika Kata ya Mahongole kwa kupanda jumla ya miti 11,000 imepandwa ikiwa Miti 6,000 imepandwa Kijiji cha Mahongole Machi 14,2025 na Miti 5,000 imepandwa leo katika Kijiji cha Kifumbe na machi 17,mwaka huu zoezi la upandaji miti 4,000 litafanyika katika Kata ya Utengule,ikiwa ni maandalizi kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya upandaji Miti Kitaifa ambapo kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yatafanyika Mkoani Njombe Machi 21,2025.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kifumbe Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo,Mhe.Mario Kihombo, ambaye ni diwani wa Kata ya Mahongole ameushukuru uongozi wa Halmashauri kwa utekelezaji wa zoezi hilo katika Kata hiyo, kwani kupitia miti hiyo kizazi cha sasa na kijacho kitapata manufaa, na kuwataka wananchi kuithamini na kuilinda miti hiyo dhidi ya majanga mbalimbali kama ukataji holela wa miti na majanga ya moto.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Makambako, Bi. Anna Mhoka amesema kuwa,katika kuhakikisha Mazingira yanasimamiwa ,kulindwa na kuendelezwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho, Halmashauri ya Mji Makambako kwa mwaka 2024/2025 inatarajia kupanda miti Mil. 1.75 kati ya Miti Mil. 1.5 ambayo TAMISEMI imeelekeza Halmashauri zote kupanda na kuwa na zidio la miti laki mbili na elfu hamsini.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kifumbe, Bw. Ferdinand Kibiki amewashukuru wananchi wa Kijiji hicho kwa ushirikiano na kujitokeza katika zoezi la upandaji miti ,na kuwataka wananchi kuwa makini na mifugo wakati miti hiyo bado midogo ili kuepusha uharibifu wa mazingira kwa mustakabali wa maendeleo ya Kijiji hicho na Makambako kwa ujumla.
Naye, Bi.Nusta Mkawala Mkazi wa Kijiji cha Kifumbe kwa niaba ya wananchi wote ameishukuru Halmashauri kupitia Kitengo cha TASAF na Kitengo cha Maliasili na uhifadhi wa Mazingira, kwa upandaji miti Kwani utawasaidia wananchi kupata faida mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mbao na nguzo ambazo zitawasaidia kukuza uchumi wa kijiji na wananchi kwa ujumla.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa