Na. Lina Sanga
Kamati ya fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Mji Makambako leo, imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha kuishia robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambayo ni ujenzi wa bweni la wavulana katika shule ya sekondari Mtimbwe unaogharimu jumla ya Mil. 154 kutoka Serikali kuu na mapato ya ndani na ujenzi wa shule mpya ya Kata ya Mjimwema kupitia mradi wa SEQUIP unaogharimu jumla ya Mil. 583.2.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako pamoja na wajumbe wa kamati hiyo, wamepongeza utekelezaji wa miradi hiyo na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassani kwani miradi hiyo itasaidia kupunguza changamoto katika sekta ya elimu na kuongeza ufaulu.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni Mkuu wa shule ya sekondari Mtimbwe, Mwl. Zuberi Kilingo amesema kuwa, jumla ya wanafunzi themanini watakaa katika bweni hilo kwani kwa sasa shule inakabiliwa na upungufu wa mabweni kutokana na ongezeko la wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanaopangiwa kusoma katika shule hiyo, hivyo bweni hilo litasaidia kupunguza changamoto hiyo pindi ujenzi ukikamilika.
Ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Mjimwema umeanza desemba 23,2024 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi machi mwaka huu na kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza baada ya kukamilisha ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na ofisi mbili,maabara ya biolojia na kemia, chumba cha TEHAMA, Maktaba moja,maabara ya fizikia, vyoo vya wavulana matundu manne, vyoo vya wasichana matundu manne na jengo la utawala.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa