Na. Lina Sanga
Kamati ya Siasa Wilaya ya Njombe imeitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Makambako (MAKUWASA) , kutenga bajeti ya upandaji miti rafiki na maji kuzunguka chanzo cha maji Fukulwa,kilichopoKata ya Mtwango pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wananchi wanaofanya shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji pamoja na viongozi katika ngazi ya Kijiji.
Maagizo hayo yametolewa leo na Wajumbe wa Kamati hiyo,katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji Makambako na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Mhe. Nusulupila Sanga,Mwenyekiti wa Kamati ya siasa Wilaya ya Njombe amesema kuwa miundombinu ya chanzo hicho cha maji ni ya muda mrefu,hivyo ili kuzuia upotevu wa maji hasa nyakati za kiangazi,ni vema jitihada za kufanya maboresho ya miundombinu hiyo zifanyike kwa kuzingatia umuhimu wa chanzo hicho ,kwani maji hayo yanahudumia wananchi wengi ikiwa ni pamoja na wakazi wa Mji wa Makambako.
Akitolea ufafanuzi wa suala la maboresho ya chanzo hicho,Meneja wa MAKUWASA,Mhandisi Oscar Lufyagilo amebainisha kuwa bajeti yenye jumla ya Mil. 27 ya kuongeza ukuta wa mto Fukulwa imetengwa na pindi ukuta huo ukijengwa utasaidia kupunguza upotevu wa maji tofauti na ilivyo sasa.
Mhandisi Lufyagilo amesema kuwa,ili kupunguza adha ya ukosefui wa maji katika baadhi ya maeneo ndani ya Mji wa Makambako,Mradi wenye thamani ya bil. 46 umeshaanza kutekelezwa ambapo jumla ya lita mil. 2 zitazalishwa kutoka mto Mgiwi uliopo mpakani mwa Wilaya ya Makete na Halmashauri ya Mji Njombe na kusafiri kupitia mabomba kwa umbali wa kilomita 90 hadi Makambako.
Aidha, Kamati ya Siasa Wilaya ya Njombe imeipongeza TASAF kwa kujenga jengo la wagonjwa wa nje na huduma ya mama na mtoto pamoja na nyumba pacha za watumishi,katika kituo cha afya cha Ikelu ambacho kitasaidia wananchi kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
Katika ziara hiyo Kamati ya Siasa Wilaya ya Njombe imekagua miradi minne ikiwa ni pamoja na mradi wa madarasa matatu na ofisi moja ya kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Maguvani,Mradi wa barabara ya Usetule na Mbugani yenye urefu wa kilomita 12.12 kwa kiwango cha changarawe,Mradi wa maji Fukulwa na mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Ikelu.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa