Na. Lina Sanga
Kamati ya siasa Wilaya ya Njombe imepongeza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa maghala 112 ya kuhifadhia nafaka unaogharimu takribani bil. 2.24,yanayojengwa katika Mtaa wa Makatani,Kata ya Lyamkena, Halmashauri ya Mji Makambako katika mfumo wa jenga,tumia na rejesha.
Pongezi hizo zilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Njombe pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo,katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Mji Makambako katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Mhe. Justin Nusupila Sanga,Mwenyekiti Kamati ya siasa Wilaya ya Njombe amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo una tija kubwa kwa wananchi na Serikali,kwani ni mradi mzuri wa uwekezaji unaowaweka wafanyabiashara pamoja kwenye mazingira rasmi na kupata soko la uhakika.
"Nipongeze utekelezaji wa mradi huu kwani una tija kwa wananchi na Serikali,na ni uwekezaji mzuri unaoenda sambamba na jitihada za Serikali kutenga maeneo rasmi ya biashara mbalimbali",alisema Mhe. Sanga.
Ametoa rai kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako,kuendelea kufanya maboresho na kukamilisha mahitaji mbalimbali ambayo yanatakiwa kufanywa na Halmashauri ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma muhimu zinazojitajika eneo la mradi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma ya Umeme inapatikana pamoja na huduma ya Maji.
Aidha,ametoa rai kwa Ofisi ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Njombe, kutenga bajeti ya matengenezo ya barabara kwenye eneo la mradi ambayo ina uwezo wa kuhimili magari mazito ya mizigo.
Leo Sanga,mbeba mizigo katika maghala hayo,ameishukuru Serikali kwa kubuni mradi huo kwani umeongeza uhakika wa watu mbalimbali kufanya kazi na kupata fedha kwa ajili ya kuendesha maisha yao.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa