Ugonjwa wa Polio ni ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Polio, ambavyo huenezwa kwa njia ya kula na kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi,na njia pekee ya kuudhibiti ugonjwa huu ni chanjo kwani mpaka sasa tiba haijapatikana.
Akizungumza katika semina ya kamati ya afya kuhusu chanjo dhidi ya polio,iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Makambako,Dr. George Kanki ambaye ni Afisa Mfuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko Nchini kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), amesema kuwa katika nchi jirani ya Malawi Mgonjwa mmoja amegundulika kuwa na ugonjwa wa polio,hivyo mikoa iliyopo karibu na Nchi hiyo inatakiwa watoto wote kuanzia umri wa miaka sifuri hadi miaka mitano lazima wapate chanjo hiyo ili kuudhibiti ugonjwa huo na kampeni hii itafanyika nyumba kwa nyumba, mtoto kwa mtoto ili kuhakikisha watoto wote wamepata chanjo na kuwekewa alama ya wino ili kurahisisha uhakiki wa watoto waliopata chanjo na ambao hawajapata chanjo.
Dr. Kanki amesema kuwa Shirika la Afya Duniani linaichukulia kampeni ya chanjo dhidi ya polio kuwa ni muhimu sana kwani ugonjwa huo unasababisha mgonjwa kupooza na kupata ulemavu wa kudumu hata kifo,na ili kuutokomeza ugonjwa huo ni lazima watoto wapewe chanjo dhidi ya polio kwa awamu nne na endapo mlipuko umetokea kama sasa haijalishi mtoto ambaye amepata chanjo zote awamu nne au moja au siku moja baada ya Mlipuko ni lazima apewe chanjo tena.
“Mgonjwa wa polio aliyepatikana Malawi ,haijulikani amepita mikoa gani na Nchi gani,huenda alifika hadi upande wa Tanzania ndiyo maana Serikali imeamua mikoa iliyo karibu na Nchi hiyo kutolewa chanjo haraka ili kuzuia maambukizi kutokea ndani ya nchi yetu,hivyo mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma watoto wote lazima wapate chanjo ili kuwakinga na maambukizi ya ugonjwa huo”,alisema Dr. Kanki.
Samweli Vianga ambaye nia Afisa afya katika Halmashauri ya Mji Makambako na Mwezeshaji katika semina hiyo,amesema kuwa kampeni ya chanjo hiyo imefanyika tofauti na miaka mingine ambapo Wazazi walikuwa na wajibu wa kuwapeleka watoto wao, katika vituo vya kutolea huduma ya afya kupata chanjo ya polio ,kwa sasa kampeni hiyo itafanyika nyumba kwa nyumba kwa sababu ya tishio la Nchi jirani ya Malawi juu ya uwepo wa Ugonjwa huo na lengo la pili ni kuwatafuta watoto chini ya umri wa miaka mitano waliopata ulemavu wa gafla (tepetepe).
Mwaka 2015 Nchi ya Tanzania ilipata cheti cha mafanikio ya kuutokomeza ugonjwa wa polio na Mwaka 2020 Bara la Afrika lilikuwa huru kwa maradhi haya ya polio na kupewa cheti kuonyesha mafanikio ya kuutokomeza ugonjwa huu katika Bara lote la Afrika baada ya Nchi ya Nigeria kukubali chanjo Dhidi ya Polio,na duniani kote ugonjwa huu ulikuwa umeshatokomezwa isipokuwa nchi mbili tu,nchi ya Pakistan na Afganistan kutokana na uwepo wa vita na pingamizi lakini dunia yote ilitarajia endapo ugonjwa wa polio ukitokomezwa katika nchi hizo mbili dunia ingekuwa imefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa polio kama ilivyofanikiwa kuutokomeza ugonjwa wa ndui.
Kampeni ya Chanjo dhidi ya polio inatarajiwa kufanyika kwa siku nne kuanzia Machi 24,2022 hadi Machi 27, 2022 katika Halmashauri ya Mji Makambako endapo mwitikio utakua hafifu kampeni hiyo itaendelea hadi kufikia malengo ya utoaji wa Chanjo hiyo.
Semina hiyo ilihudhuriwa na Afisa Mpango wa Taifa wa chanjo kutoka Wizara ya Afya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Njombe,Mkuu wa Polisi wilaya ya Kipolisi Makambako(OCD),Viongozi wa madhehebu ya Dini mbalimbali,Mwakilishi wa Wafanyabiashara,Mwakilishi wa Wataalamu wa tiba asili pamoja na wataalamu wa Idara mbalimbali katika Halmashauri ya Mji Makambako.
Mwisho.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa