Na. Lina Sanga
Chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa Miaka mitano awamu ya pili inatarajiwa kuanza kutolewa kesho Aprili 28,2022 hadi Mei 1,2022,katika Halmashauri ya Mji Makambako,nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha watoto wote wenye umri huo wanapata chanjo hiyo lakini pia kuwafikia watoto wenye ulemavu wa viungo mbalimbali hasa ambao wamefichwa na kushindwa kufikiwa kiurahisi.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Makambako, Dr. Alexander Mchome katika kikao cha Kamati ya Msingi ya Afya Ngazi ya Jamii (PHC), kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji Makambako.
Dr. Mchome amesema kuwa katika utaratibu wa kawaida Chanjo ya polio inatolewa kwa watoto wenye umri wa miaka mitano kwa njia ya matone kwa awamu nne kuanzia anapozaliwa,baada ya wiki sita,wiki kumi na wiki kumi na nne tangu mtoto azaliwe, kwa sasa inatolewa kwa awamu nne pia kwa kila mtoto ikiwa ni kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa polio tangu kutokee tishio la uwepo wa mgonjwa wa polio Nchini Malawi ili kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa huo.
Aidha Dr. Mchome kupitia Idara ya Afya amesema wamejipanga kutoa elimu kwa jamii,kuhamasisha na kuelewesha watu kuhusu ugonjwa wa polio na umuhimu wa chanjo ya ugonjwa huo ili kupata ushirikiano wa kutosha na kujitoa katika kuhakikisha jamii inakuwa salama.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Njombe, Emanuel George ametoa wito kwa wananchi wote kuachana na dhana potofu juu ya chanjo ya polio inayotolewa kwa watoto na chanjo ya Uviko 19,kwani chanjo zote ni muhimu kwa watu wote,hivyo kila mtu anawajibu wa kujitokeza kupata chanjo ya Uviko 19 na kuhakikisha watoto nao wanapata chanjo ya polio ili jamii nzima ibaki salama.
“Chanjo ya Uviko 19 watu wote wanatakiwa kupata chanjo hiyo isipokuwa kwa baadhi ya watu wanaohitaji uangalizi maalumu wa daktari kutokana na sababu za kiafya ,na hakuna kigeni chochote katika chanjo zote zinazotolewa Nchini kwani tangu miaka kadhaa iliyopita chanjo nyingi zimetolewa nab ado zinaendelea kutolewa kama chanjo ya Surua,chanjo ya Polio na chanjo ya homa ya ini ambayo watu wengi wanaipuuza kwa sababu huenda bado hawajamuona mgonjwa anayesumbuliwa na ini au hawajaamua kufuatilia kiundani kuhusu athari za ugonjwa huo”, alisema bw. George.
Naye Baldwin Mkalula mwakilishi wa paroko kutoka kanisa la Romani katholik Makambako, ametoa rai kwa wananchi wote pamoja na Mamlaka mbalimbali kutoishi kwa mazoea bali kila mmoja ahakikishe anaishi katika misingi ya maisha kila siku ikiwa ni pamoja na suala la usafi,kwani Ugonjwa wa polio unaambukizwa kwa njia ya kinyesi lakini pia ugonjwa wa Uviko 19 nao unaambukizwa kwa kugusana au kushikana,hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha ananawa mikono kwa maji safi yanayotiririka pamoja na sabuni ili kuzuia maambukizi.
Katika awamu ya kwanza ya kampeni ya utoaji wa Chanjo ya Polio katika Halmashauri ya Mji Makambako jumla ya watoto 22,218 sawa na asilimia 144 walipata chanjo hiyo na Halmashauri ya Mji Makambako kushika nafasi ya kwanza kati ya halmashauri sita zilizopo katika mkoa wa Njombe na kushika nafasi ya pili kwa upande wa Mikoa ya nyanda za juu kusini ikiwa ni pamoja na mkoa wa Mbeya,Ruvuma na Iringa.
Aidha, Halmashauri ya Mji Makambako inatarajia kutoa chanjo ya homa ya ini kwa wananchi wote ambapo tofauti na chanjo nyingine,chanjo hiyo inalipiwa na mwananchi anayehitaji,Homa ya ini ni ugonjwa unaoambukizwa kupitia kwenye damu na majimaji mengine ya mwili kama jasho.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa