Na. Lina Sanga
Njombe
Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa watu binafsi kufungua kampuni za utalii katika Mikoa ya Kusini,na kufanya shughuli za utalii katika mkoa wa Njombe pamoja na wawekezaji katika kilimo cha maua kwani hali ya hewa ya mkoa wa Njombe na Miundombinu inaruhusu.
Mhe. Mtaka ametoa wito huo leo katika hafla ya uzinduzi wa mikakati ya kutangaza utalii kusini mwa Tanzania,iliyofanyika leo katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Amesema kuwa,Mkoa wa Njombe una hifadhi ya kitulo yenye maua mazuri,na kwa sasa soko la maua limekuwa hafifu na wawekezaji wa maua wameanza kwenda Nairobi kununua Maua.
Ametoa wito kwa wawekezaji wa kilimo cha maua kuwekeza Njombe kwani hali ya hewa ni rafiki,pia kuna vivutio vingi ikiwemo hifadhi ya kitulo na safu ya milima kipengere.
Ameongeza kuwa,utalii uliopo mikoa ya Kaskazini haukujiumba bali umejengwa na watu binafsi,hivyo utalii unajengwa na sekta binafsi ,Serikali ina jukumu la kuweka miundombinu na mazingira wezeshi.
Aidha amewataka wananchi wa Mkoa wa Njombe kuchangamkia fursa mbalimbali za utalii na kujipatia kipato,kwani baada ya miaka mitatu Mkoa wa Njombe hautarajii kuwa na wanufaika wa Tasaf wanaotokana na uzembe.
“Mhe. Pindi Chana anakuja anakwambia kilimo cha miti hulimi,,utalii hufanyi,viazi tunalima siku sitini hulimi,ngano siku sitini na tano hulimi,mchicha siku ishirini na moja hulimi,tunajenga shule usome bure husomi unakaa unasubiri Rais awape hela kutoka mbinguni,umezeeka nipo Tasaf kwa uzembe,kizazi hichi cha Tasaf ni cha mwisho hakuna hela ya Tasaf atayopewa mzembe labda kwa mlemavu wa viungo na tunaanza kutunza kumbukumbu kwenye mfumo wa kidigitali ”, alisema Mhe. Mtaka.
Amemuomba Waziri wa Maliasili na utalii kuziruhusu bodi kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Njombe,ili kusaidia kuvitangaza vivutio hivyo,pamoja na kujifunza masuala mbalimbali ya utaliii kama vile nyumbu wanaohama kutoka Kenya kuja Tanzania pamoja na ndege wanaotoka Ulaya kuja hifadhi ya Kitulo iliyopo Makete.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa