Kata ya lyamkena iliyopo katika halmashauri ya Mji Makambako,imeibuka kinara katika zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 19, ya J&J kwa kuvuka lengo la utoaji chanjo kama ilivyokadiliwa kutoa chanjo 126, zilizotolewa kwa kila kata katika halmashauri ya Mji makambako ,kutokana na mwamko Mdogo wa wananchi waliokuwa wanajitokeza kupata chanjo.
Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Makambako, Dkt. Alexander Mchome katika kikao cha tathmini ya zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 19 ,katika halmashauri ya Mji Makambako na utambulisho wa chanjo ya Sinopharm.
Dkt. Mchome amesema kuwa kata ya Lyamkena imefanikiwa kuchanja jumla ya watu 185, na kufuatiwa na kata ya Mlowa ambayo imetoa chanjo 169 na kata ya Kitandililo imetoa chanjo 113 kati ya chanjo 126 ambazo zilitolewa kwa kila kata.
Akielezea jitihada zilizofanyika na kusaidia kutoa chanjo hizo,Diwani wa kata ya Lyamkena,Mhe. Salumu Mlumbe amesema kuwa kuitisha mikutano ya hadhara katika mitaa na kuwapa elimu wananchi kuhusu chanjo na viongozi wa kata kupata chanjo imesaidia kuwaaminisha wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama na kuamua kuchanja baada ya kuona viongozi wao wanaowaongoza wamechanja na hawajapata madhara yoyote.
Dkt. Mchome ametoa wito kwa wakazi wa Halmashauri ya Mji Makambako,kujitokeza katika vituo vya kutolea chanjo ili kupata chanjo badala ya kusubiri kufuatwa kwenye makazi yao,kwani kwa kufika kituoni ni rahisi zaidi katika kufanikisha zoezi hilo tofauti na kumfuata mtu mmoja mmoja,lakini inapobidi kuwafuata watu kwenye maeneo ya wataalamu wa afya watafanya hivyo.
Aidha amewataka wananchi ambao hawajapata chanjo ya J&J kujitokeza kupata chanjo ya sinopharm, ambayo imeletwa Nchini kutoka Nchini China baada ya chanjo ya J&J kuisha.
Akitolea ufafanuzi wa chanjo hiyo,Dkt Mchome amesema kuwa Chanjo ya sinopharm na J&J zote zinafanya kazi moja ya kuzalisha kinga dhidi ya kirusi cha UVIKO 19,tofauti yake ni utaalamu namna ya utengenezaji,ndio maana sinopharm ili mtu apate kinga kamili ni lazima apate dozi mbili za chanjo ambapo dozi ya pili itatolewa baada ya siku ishirini na nane tofauti na J&J ambayo inatolewa dozi moja tu.
“Chanjo ya sinopharm imetengenezwa na kirusi kilichouliwa kwa kemikali na kuondolewa uwezo wa kuambukiza ugonjwa wa UVIKO 19 kwa binadamu,na endapo mtu huyo akipata maambukizi ya UVIKO 19,mwili unakuwa salama kwa sababu chanjo aliyopata inatengeneza kinga za kuulinda mwili dhidi ya ugonjwa huo,na baada ya kuchoma chanjo ya sinopharm basi mtu huyo hatakiwi kuchoma chanjo ya aina yoyote hadi siku 14 tangu kuchoma chanjo ”alisema Dkt. Mchome.
Halmashauri ya Mji Makambako imepokea jumla ya chanjo 2100 za sinopharm,ambazo zitatolewa kwa watu wenye umri kuanzia miaka kumi na nane,kina mama wajawazito,wazee na hata watu wenye magonjwa mengine kwani wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya UVIKO 19 kama watu wenye magonjwa ya moyo,kisukari,figo,shinikizo la damu na Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI).
Watu wenye mzio na baadhi ya vitu vilivyotumika kutengeneza chanjo ya sinopharm hawatapata chanjo hii pamoja na watu ambao watagundulika kuwa na maambukizi ya UVIKO 19 hawatapata chanjo ya sinopharm hadi miezi sita baada ya kupata matibabu na kupona ugonjwa wa korona.
MWISHO.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa