Halmashauri ya Mji wa Makambako inatekeleza afua mbali mbali za lishe kwa kuzingatia viashiria vilivyomo katika mkataba wa lishe, Lengo ni kuhakikisha huduma bora za Lishe zinatolewa kwa walengwa/jamii ili kuondokana na matatizo ya utapiamlo hususani udumavu .
Mkoa wa Njombe unaongoza kwa kuwa na watoto wengi wenye ukosefu wa Lishe bora (Udumavu, ukondefu, uzito pungufu, n.k.) Kikao cha Kamati ya Lishe cha tarehe 24/03/2020 kilijadili : Taarifa ya utekelezaji wa Maazimio ya kikao cha Kamati ya Lishe ya Halmashauri kilichofanyika tarehe 29/11/2019, Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha robo ya pili Oktoba - Disemba 2019/2020,Taarifa ya utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa lishe kipindi cha pili Oktoba - Disemba 2019/2020.
Taarifa ya utekelezaji wa Maazimio ya kikao cha Kamati ya Lishe ya Halmashauri kilichofanyika tarehe 29/11/2019
Utekelezaji wa maazimio ya Kikao cha Kamati ya Lishe kilichofanyika tarehe 29/11/2019, ulifanyika kama ifuatavyo:
1. Kuhakikisha akina mama wajawazito wanapata kiwango sahihi cha madini chuma na asidi ya foliki: Idara ya afya kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa akina mama wajawazito kuwahi kuanza/kuhudhuria kliniki ili kuweza kupata nyongeza ya madini chuma na asidi ya foliki kwa kiwango sahihi kupitia wahudumu wa vituo vya kutolea huduma za afya,wahudumu ngazi ya jamii; kupitia mikutano ya vijiji/mitaa na kwenye nyumba za ibada na Radio(ICE FM).
2. Kuhakikisha watoto wenye utapiamlo mkali wanatambuliwa mapema na kupatiwa matibabu: Kuendelea kushirikiana na serikali ya Vijiji/Mitaa pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kuweza kuwabaini mapema watoto wote wenye utapiamlo na kupewa rufaa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupata matibabu.
3. Idara ya elimu kushirikiana na afisa lishe watoe elimu katika shule za msingi kuhusu mpangilio wa vyakula ili kukidhi mahitaji ya lishe kwa wanafunzi: Elimu ilitolewa katika shule 14 kati ya 42 za Msingi kipindi cha robo ya pili 2019/2020(Ibatu,Mlenga,Kitandililo,Nyamande,Usetule,Mahongole,Manga,Kifumbe,Kahawa,Mashujaa,Juhudu,Nyambogo,Ikelu na Mtanga) Aidha shughuli ni endelevu.
4. Kuhakikisha kila idara imetenga fedha za utekelezaji wa afua za lishe kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa katika kikao cha maandalizi ya awali ya mipango na bajeti za afua za lishe kwani suala la lishe ni mtambuka: Idara husika zimezingatia agizo hilo ambapo jumla ya fedha zimetengwa kwa utekelezaji wa afua za lishe kwa mwaka 2020/2021.
Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha robo ya pili Oktoba - Disemba 2019/2020
Utekelezwaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha robo ya pili Oktoba-Disemba 2019/2020 ulifanyika kama ifuatavyo:
1. Kufanya maadhimisho ya mwezi wa afya na lishe ya mtoto kwa kutoa matone ya Vitamin A na dawa za minyoo na upimaji wa hali ya lishe kwa watoto wa miezi 6-59: Jumla ya watoto 14,675 wenye umri miezi 6-59 walipata matone ya Vitamini A, ambapo walengwa walikuwa 13,682(107%). Watoto 11887 kati ya 12057(98%)walipewa dawa za minyoo na kupimwa hali za lishe.
2. Kufanya kikao cha maandalizi ya awali ya mipango na bajeti za afua za lishe: Wajumbe wa kamati ya lishe 22 walijengewa uwezo na wataalam kutoka OR-TAMISEMI namna sahihi ya kuandaa mipango na bajeti za afua za lishe ili kukabiliana na matatizo ya lishe duni kwa jamii.
3. Kufanya maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya kijiji/mtaa: Siku za afya na lishe ya kijiji zilifanyika katika mitaa 3(Magegele,Kilimahewa, na vijiji 2(Ibatu na Utengule) ambapo jumla ya watoto
359 walipimwa urefu ili kubaini kiwango cha udumavu ambapo watoto 13 (3.6%)wamedumaa.
4. Kufanya ufuatiliaji wa huduma za lishe katika vituo 11 vinavyotoa huduma za afya ya uzazi na mtoto ifikapo Juni 2020: Watoa huduma za afya 16 kutoka vituo 7 walijengewa uwezo kwenye ujazaji wa takwimu za lishe,ufuatiliaji wa ukuaji na maendeleo ya mtoto na unasihi wa lishe ili kuboresha huduma.
5. Kufanya kikao cha kamati ya lishe ya Halmashauri kwa kipindi cha robo ya pili mwaka2019/2020: Kikao kimefanyika.
Changamoto
Uhaba wa vidonge vya kuongeza wekundu wa damu kwa akina mama wajawazito katika vituo vya kutolea huduma za afya zinazomilikiwa na taasisi za dini na vituo binafsi hivyo kupelekea halmashauri kuwa na kiwango kidogo cha utoaji wahuduma hiyo.
Maazimio yaliyotolewa na wajumbe kwenye Kikao cha Kamati ya Lishe cha Tarehe 24/03/2020
1. Kuendelea kutoa elimu ya Lishe bora kuanzia wanafunzi wa shule za misingi mpaka sekondari ili kupunguza tatizo la utapiamlo linalosababisha udumavu wa watoto.
2. Afisa Lishe wa halmashauri ashirikishwe katika kila kikao cha walimu na wazazi ili awe anatoa elimu ya Lishe bora.
3. Maafisa Elimu msingi na Sekondari kwa kushirikiana na Afisa Lishe waandae mpango kazi wa kwenda kuwafundisha wanafunzi(Msingi na Sekondari) Elimu ya Lishe bora.
4. Jamii iendelee kupata Elimu ya Lishe bora kupitia maafisa Lishe waliopo kwenye maeneo yao.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa