Na. Lina Sanga
Kutokana na kupanda bei ya pembejeo za kilimo hususani mbolea,Serikali imeanza kusajili wafanyabiashara wa mbolea na wakulima ili kila mkulima aweze kupata mbolea yenye ruzuku.
Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Makmbako, Mhe. Deo Sanga leo katika mkutano wa hadhara kwenye vijiji vitatu vilivyopo Kata ya Utengule katika Halmashauri ya Mji Makmbako ikiwa ni ziara yake ya kijiji kwa kijiji,Mtaa kwa Mtaa ili kuongea na wananchi,kusikiliza kero zao na kutoa jumbe mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Ujumbe wa Sensa ya watu na Makazi 2022,Mbolea ya ruzuku na bajeti ya Serikali.
Mhe. Sanga amesema kuwa,mfumo wa uuzaji wa mbolea ya ruzuku ya sasa ni tofauti na uliopita,kwani ruzuku zilizopita walipata wakulima wachache lakini kwa sasa Wizara ya kilimo watawatembelea wakulima katika mashamba yao na kupitia idara ya kilimo watawasajili wakulima kupitia Mwenyekiti wa eneo husika ili kupata idadi kamili za ekari za shamba kwa kila mkulima na kila mkulima atapata kulingana na ukubwa wa shamba lake aliloandikishwa.
Amesema kuwa kupitia takwimu hizo zitazopatikana kupitia Mwenyekiti Serikali itazitumia kuleta ruzuku katika maduka ambayo wakulima wa maeneo hayo wataenda kununua,hivyo mkulima atapata mbolea kwa bei ya punguzo.
“Endapo imetambulika kuwa kuna ekari 300 za watu zinazohitaji UREA kadhaa na DAP kadhaa,kwa hiyo Serikali itatoa ruzuku kule unakokwenda kununua,ukienda kununua hapo bei inakuwa imeshapunguzwa Mama Samia ameshaweka hela yake pale”,alisema Mhe. Sanga.
Ameongeza pia Serikali kupitia Mama Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania imeleta mwekezaji,ambaye ameshajenga kiwanda jijini Dodoma cha kutengeneza Mbolea ya UREA,DAP,CAN na aina nyingine na ujenzi wa kiwanda hicho umekamilika kwa asilimia 98 na kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Agosti mwaka huu,hivyo bei ya mbolea itapungua zaidi.
Mhe. Sanga ametoa wito kwa wakulima wote kutoa taarifa sahihi za mashamba wanayolima na kujiandikisha ili waweze kupata mbolea za ruzuku.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa