Na. Lina Sanga
Jana Julai 25,2023 ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya Mashujaa,Halmashauri ya Mji Makambako ilifanya maadhimisho hayo ,katika baadhi ya shule za sekondari na msingi ili kuwajengea uelewa wanafunzi juu ya umuhimu wa siku hiyo na umuhimu wa uzalendo kwa maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.
Afisa Michezo wa Halmashauri ya Mji Makambako ,Taifa Lumato akizungumza na wanafunzi hao na kuelezea historia fupi ya mashujaa nchini na umuhimu wao,alitoa wito kwa wanafunzi na wananchi wote nchini,kutambua umuhimu wa maadhimisho ya siku ya mashujaa na kuwaenzi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuikomboa nchi yetu na kuiweka salama, hivyo kila mtu yampasa kuwa mzalendo na kujitoa kwa ajili ya taifa.
Ametoa wito kwa walimu wa masomo ya historia na uraia kuendelea kutoa Elimu juu ya historia ya mashujaa, ili kuwajengea wanafunzi hao moyo wa uzalendo na kujitoa kwa ajili ya nchi yao kwani ndio taifa la kesho.
Naye,Afisa utamaduni wa Halmashauri ya Mji Makambako, Ester Mwakalindile ,alisema kuwa maadhimisho ya siku ya mashujaa yanayofanyika julai 25,kila mwaka kwa lengo la kukumbushana historia ya mashujaa , waliojitoa kwa ajili ya taifa pasipo kujali uhai wao ,kwa maslahi ya taifa lote kwa kutanguliza uzalendo mbele kwani bila uzalendo nchi ingevamiwa na kuendelea kutawaliwa.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika shule ya sekondari Makambako , Deo Sanga , shule ya msingi Mashujaa na Azimio, kwa kuimba nyimbo za kizalendo , kufanya usafi wa mazingira na kumwagilia miti ili kuwaenzi mashujaa hao akiwemo hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere aliyepigania uhuru wa Tanganyika.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa