Na.Lina Sanga
Dodoma
Maafisa habari wa Mikoa,Halmashauri na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi licha ya Changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Charles Msonde katika kikao kazi cha Maafisa habari wa Mikoa,Halmashauri na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kilichofanyika jana Jijini Dodoma, katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Msonde amesema kuwa changamoto ni mchakato wa maendeleo,na panapokuwa na changamoto tunaitafuta fursa ya changamoto na ikitatuliwa tunapiga hatua kubwa ya maendeleo hivyo maendeleo ni mchakato wa kutatua changamoto zilizopo.
"Mhe. Waziri Maafisa habari hawa wanakabiliwa na changamoto.mbalimbali baadhi ni kukosa umuhimu kwenye mamlaka zao kutokana na baadhi ya wenye mamlaka kupuuza umuhimu wa maafisa habari,kutumika nje ya taaluma zao, mamlaka zao kutofanyia kazi maelekezo yanayotolewa na ofisi ya Rais TAMISEMI ya kuwatumia maafisa habari kuhakikisha wanashiriki shughuli mbalimbali za maendeleo na miradi, kuwaruhusu kuingia katika vikao vya kisheria ili kuwawezesha kutambua mambo mbalimbali ya muhimu ya kuwaelimisha na kuwaeleza wananchi wetu lakini pia maafisa habari wenyewe kukosa weledi katika Utekelezaji wa majukumu yao",amesema Msonde.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imetekeleza kazi nyingi kuwaletea maendeleo wananchi hivyo jukumu la Maafisa habari ni kuhabarisha umma juu ya kazi na miradi mbalimbali iliyotekelezwa na ambayo inatarajiwa kutekelezwa Serikali hapa nchini.
Ameongeza kuwa anatambua maafisa habari wamepewa wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanajitambua wenyewe, kufahamu majukumu yao na kutekeleza majukumu yao kwa weledi , kuhakikisha maendeleo ya nchi na yanayofanyika na haki ya wananchi ya kupata habari inapatikana kwa kuzingatia sheria,kanuni na miongozo ya Serikali iliyopo.
Msonde amesema kuwa lengo kuu la kikao kazi hicho ni kuwapitisha maafisa habari katika miongozo mbalimbali,na kutambua mambo makubwa ambayo Serikali inafanya kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Katika kikao kazi hicho cha Maafisa habari miongozo mbalimbali ilitolewa ikiwa na miongozo ya utekelezaji wa miradi ya elimu, utekelezaji wa miundombinu ya afya,Sura ya bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI,Taasisi na Sekretariet za Mikoa na Halmashauri,Majukumu ya idara ya Serikali za Mitaa,Uanzishwaji wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Usimamizi wa tovuti za Serikali na mitandao ya kijamii.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa