Na. Lina Sanga
Njombe
Maafisa lishe Mkoa wa Njombe wametakiwa kutumia Mbinu mbadala kutoa elimu kwa wanawake,Vijana na watoto kuhusu masuala ya Unyonyeshaji,afya ya uzazi na matumizi sahihi ya dawa za uzazi wa mpango na dawa za kuongeza nguvu za kiume na athari za matumizi holela ya dawa hizo katika umri mdogo.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka katika kikao cha utiaji saini mikataba ya lishe kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe,ambapo imedaiwa kuwa Mkoa wa Njombe unakabiliwa na lishe duni kwa watoto hali inayopelekea watoto kupata udumavu.
Mhe. Mtaka amesema kuwa,ipo haja ya maafisa lishe kutoa elimu ya lishe kwa jamii hasa kwa wanawake juu ya faida ya unyonyeshaji,kwa kubuni mbinu mbadala ya kuwapata wanawake na kina mama wanao nyonyesha ili kuwapa elimu hiyo, kwa kuwafata kwenye makongamano ya dini na shuleni kwa ajili ya kuwapa elimu ya lishe wanafunzi ikiwa ni pamoja na athari za matumizi holela ya madawa ya kuongeza nguvu za kiume kwa vijana wa kiume na dawa za kuzuia ujauzito (P2) kwa watoto wa kike.
Amesema kuwa,matumizi ya madawa hayo kwa sasa yamekithiri kwa watoto wadogo bila kufikiria athari wanazoweza kuzipata baada ya miaka kadhaa,hali hii inaweza kuleta kizazi cha ajabu miaka ijayo.
“Kijana ana miaka 15 anatumia dawa za kuongeza nguvu za kiume mara vumbi la kongo ili kumuonyesha ufundi rafiki yake wa kike wala sio mke,kijana akifika miaka 35 amechoka na huenda akapata madhara hadi kwenye ubongo,binti wa miaka 15 anatumia dawa za kuzuia mimba akifika umri wa kuzaa nini kitatokea?ipo haja ya elimu hii kuwafikishia walipo”,alisema Mhe. Mtaka.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kuzungumza na watoto wao juu ya matumizi ya dawa za kuzuia mimba na dawa za kuongeza nguvu za kiume, pamoja na athari zake kwa kutambua wakati sahihi wa kuzungumza na watoto kuhusiana masuala ya afya ya uzazi na kuwataka wanawake kuacha tabia ya kutonyonyesha watoto kwa kuepuka ulaji wa vyakula vyenye afya kwa mtoto kwa kuhofia kunenepa au kuongeza uzito,hali inayosababisha mtoto kupata lishe duni.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa