Na.Tanessa Lyimo
Halmashauri ya Mji Makambako jana imetoa mafunzo ya mtaala mpya ngazi ya shule, ikiwahusisha walimu wakuu 17 na walimu wa darasa la awali 17 kutoka kwenye baadhi ya shule kati ya shule za msingi 57 zilizopo katika Halmashauri ya Mji Makambako baada ya mafunzo ngazi ya Halmashauri kukamilika.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika shule ya msingi Sigrid, Mkuu wa divisheni ya elimu ya awali na msingi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Mwl.Samwel Komba amewataka walimu waliohudhuria mafunzo hayo kuyapokea mafunzo ya mtaala mpya kikamilifu ili waweze kuwaelekeza walimu wengine ili kukamilisha mafunzo hayo.
Aidha, amewasisitiza walimu kutumia nafasi hiyo iliyotolewa na waratibu na wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) ,kwa kushirikiana na Halmashauri katika kuleta chachu ya utekelezaji wa mtaala mpya kwani mabadiliko ya sera, ukuaji wa Sayansi na Teknolojia umehamasisha jamii kupata mwamko katika kuhakikisha kizazi cha sasa kinaandaliwa vyema kujikomboa kwa mahitaji ya dunia ya sasa na baadae.
Kwa upande wake mratibu wa Mafunzo hayo Kitaifa katika Mkoa wa Njombe ,Mwl. Borgias Ntamwana kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI divisheni ya Elimu, amewapongeza walimu kwa ushiriki wao na kuwasisitiza kuzingatia matumizi mazuri ya muda katika semina hiyo ili kuwasaidia kukusanya Zana na tunu mbalimbali katika kuwarahisishia uelewa wakati wa mabadiliko wa mtaala huo.
Mwl. Jerome Mwakifuna, mwezeshaji Kitaifa kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI,ameishukuru Halmashauri na walimu kwa maandalizi na utayari wa mapokeo ya semina ya mafunzo ya mtaala mpya hali inayodhihirisha uwepo wa utayari wa kujipanga vyema katika kufanikisha maboresho ya mtaala huo.
Naye mkuu wa shule ya msingi Magegele, Mwl. Amos Mtawa ambaye ni miongoni kati ya timu ya uwezeshaji ngazi ya Halmashauri ,amesema mafunzo hayo yatawasaidia walimu katika kumpa ujuzi mwanafunzi mwenye umri wa miaka 5 wakati anapoanza elimu ya awali kujitambua, kujithamini na kufanikisha ndoto katika maisha yake.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa