Na. Lina Sanga
Wanafunzi wa shule ya Msingi Magegele wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe Samia Suluhu Hassan kwa Fedha zilizotolewa kwa ajili ya Ujenzi wa Kisima kirefu cha Maji shuleni hapo na kuwasaidia kutobeba vidumu vya maji kutoka nyumbani kwa ajili ya matumizi ya vyooni,kudekia, kumwagilia maua na bustani za mboga.
Hayo yamebainishwa na wananafunzi wa shule hiyo wakati wakizungumza na Mbunge wa jimbo la Makambako,Mhe. Deo Kasenyenda Sanga maarufu kama Jah people alipotembelea shule hiyo leo kwa ajili ya ukaguzi wa ujenzi wa madarasa mawili yaliyojengwa na Asas.
Akizungumza na wanafunzi hao Mhe. Sanga amesema kuwa kama mwakilishi wa wananchi wa jimbo la makambako,alifikisha ujumbe kwa Mhe. Samia ili kuwasaidia wanafunzi kutobeba maji kutoka nyumbani maji yatoke shuleni na suala hilo limefanikiwa.
"Zamani mlikua mnabeba vidumu vya maji kutoka nyumbani kila siku,lakini Mhe. Samia aliposikia ombi langu la kuchimbwa kisima cha maji hapa shuleni ili kuwapunguzia mzigo wa kubeba maji kila siku alilipokea na ametuletea fedha na sasa maji yanatoka shuleni hapa vidumu sasa basi",alisema Mhe. Sanga.
Ametoa wito kwa wanafunzi kulinda miundombinu ya madarasa na vitu vilivyopo katika shule hiyo,na kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzie na watoe taarifa endapo kuna mtu anataka kuharibu miundombinu ya shule.
Pia amewataka wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii kwa kuiga mfano wa Mama samia kwani wakifaulu vizuri , watapata nafasi ya kushika nyadhifa mbalimbali kwani sasa hivi viongozi wakubwa wengi ni wanawake.
Jumla ya shilingi mil. 32.8 zilipokelewa kwa ajili ya uchimbaji wa kisima kirefu pamoja na uwekaji wa miundombinu ya maji katika shule ya Msingi Magegele,ikiwa ni moja ya miradi iliyotekelezwa kwa fedha za ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 .
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa