Na. Lina Sanga
Njombe
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeshauriwa kutafuta namna ya kuwafidia wakulima waliouziwa mbolea zilizochakachuliwa katika msimu wa kilimo wa 2022/2023, kutokana na hasara walizosababishiwa na wauzaji wa mbolea wasio waaminifu,kufanya marekebisho ya sheria ya mbolea,pamoja na kuwezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa ya ukaguzi wa mbolea kabla ya kufika shambani.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa katika kikao na Mkurugenzi Mkuu wa TFRA,Dkt. Stephan Ngailo,kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji Njombe na kuhudhuriwa na Viongozi na wataalamu wa Halmashauri za Wilaya ya Njombe.
Mhe. Kissa amesema kuwa, njia ya ukaguzi wa mbolea inayotumika kwa sasa na Maafisa Kilimo ya kutumia kifaa chenye ncha kutoboa mfuko,imepitwa na wakati na baadhi ya Mawakala hukataa kutobolewa kwa mifuko , hali inayotoa mwanya kwa wachakachuaji kukamilisha adhma yao.
Dkt. Stephan Ngailo,Mkurugenzi Mkuu wa TFRA amesema kuwa, marekebisho ya sheria ya mbolea yanaenda kufanyika ili kuhakikisha usalama wa mbolea na kuongeza adhabu kwa wakiukaji wa sheria hiyo ambao kwa sasa walikuwa wanafutiwa leseni na kulipa faini isiyopungua Mil. 100.
Aidha, amesema kuwa usajili wa wakulima ambao hawakujisajili msimu uliopita umeanza pamoja na kuhuisha taarifa za usajili wa wakulima wote, ili kupata taarifa sahihi pamoja na usajili wa vyama vya ushirika vinavyoaminika ili vitumike kusambaza mbolea ifikapo Julai 1,2023.
Ametoa wito kwa wakulima kuanza kujisajili mapema kwa kutoa taarifa sahihi ,ikiwa ni pamoja na idadi ya ekari za mashamba wanazolima pasipo kuogopa,idadi ya misimu wanayolima kama ni miwili au mmoja, ili wapate mbolea wanazohitaji mapema kabla ya msimu wa kilimo haujanzaa na kuwatoa hofu wakulima wadogo hususani wa bustani kuwa, mbolea zitapatikana kwa ujazo wa kuanzia kilo 5 na kuendelea ili hata wakulima wadogo waweze kununua.
Amezitaka Halmashauri kuainisha vituo vya kusambazia mbolea pamoja na maghala ya Serikali ,ambayo hayatumiki ili mwezi Julai mbolea zianze kutolewa na kuwafikia wakulima kwa wakati na kuwataka wataalamu wa Kilimo kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wananchi ili kuondoa dhana potofu kuwa kuwa mbolea inaharibu ardhi.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa