Na. Lina Sanga
Wananchi wametakiwa kuhudhuria mahakamani kutoa ushahidi wa Kesi za unyanyasaji wa wanawake na watoto,ili watuhumiwa watiwe hatiani na kupata adhabu kwa makosa yao.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya kipolisi Makambako (OCD),Afande Omary Diwani katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika jana katika ukumbi wa mikutano halmashauri ya Mji Makambako.
Afande akijibu hoja ya Mhe. Stella Uhemba ambaye ni diwani wa Viti maalum baada ya kuhoji kwanini watuhumiwa wasifungwe ili wengine wajifunze,kwani matukio 57 ya unyanyasaji wa wanawake na watoto katika halmashauri ya Mji Makambako yaliyoripotiwa ni mengi na bado yanaongezeka.
Afande Omary amesema kuwa polisi haina mamlaka ya kumfunga mtuhumiwa yeyote bali mahakama,lakini kumekuwa na changamoto ya ushahidi kwani watu wengi hawafiki mahakamani kutoa ushahidi kwa sababu watuhumiwa ni ndugu na jamaa zao wa karibu,na kusababisha mtuhumiwa kuachiwa huru na matukio ya unyanyasaji kuendelea kuongezeka kwa kasi.
Ametoa wito kwa Waheshimiwa Madiwani na Watendaji kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuachana na vitendo vya unyanyasaji, kwani ni kinyume na haki za binadamu.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Makambako, Mhe. Hanana Mfikwa ametoa wito kwa wazazi,viongozi wa dini na wazee wa mila kushiriki malezi bora ya watoto katika jamii,na kuwaelimisha juu ya vitendo vya unyanyasaji na kutoa ushahidi mahakamani ili watuhiwa wachukuliwe hatua kwani takwimu ya matukio hayo ni kubwa sana.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa