Na. Lina Sanga
Mbeya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Kilimo,kuhakikisha mbolea ya ruzuku inaanza kutolewa agosti 15 ili kuwawezesha wakulima kulima kwa wakati kulingana na msimu.
Mhe. Samia ametoa agizo hilo leo katika kilele cha maonyesho ya nanenane kwa mwaka 2022,yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya,baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa mbolea ya ruzuku iliyowasilishwa na Waziri wa Kilimo,Mhe. Hussein Bashe.
Pia amezitaka kampuni zote zinazosambaza mbolea ya ruzuku,kutangaza mawakala wake ambao wanauza mbolea yenye ruzuku ili wakulima wajue.
Ametoa Wito kwa wakulima wote kujisajili ili waweze kupata mbolea ya ruzuku,na siku za mbeleni vitambulisho vya wakulima vitatolewa ili kuwawezesha wakulima kupata ruzuku mbalimbali na mikopo katika taasisi za kifedha.
Aidha,ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuwagawia mashamba yenye hatimiliki vijana,ili kuwawezesha kujiajiri kupitia sekta ya kilimo lakini pia kuwawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha na kuagiza Kila mkoa kutenga maeneo makubwa kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa na sio vipande vipande.
Pia Mhe. Samia Suluhu Hassan amekabidhi funguo za trekta kwa wakulima bora wawili na ameshuhudia utiaji saini mikataba 21 ya miradi ya Kilimo yenye thamani ya zaidi ya bil. 180 itayotekelezwa kwenye Mikoa 7,Wilaya 12, yenye ukubwa wa hekta 26,700 na miradi hiyo ikikamilika jumla ya ajira mpya zaidi ya laki moja zitaongezeka na kuongeza uzalishaji wa zaidi ya tani 97,000 za mpunga.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa