Na. Lina Sanga
Mbunge wa jimbo la Makambako,Mhe. Deo Kasenyenda Sanga amesema ataishauri bodi ya Maji ya Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Makambako (MAKUWASA),juu ya gharama za maji kwa matumizi nje ya matumizi ya nyumbani ikiwa ni pamoja na ufyatuaji wa tofali.
Mhe. Sanga ameyasema hayo leo katika Mtaa wa Kilimahewa,wakati akijibu maswali na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wananchi hususani katika Sekta ya Maji.
Amesema kuwa,kutokana na sheria za maji na gharama za utoaji wa huduma za maji majumbani,ni vema bodi ya maji ione namna ya kuwasaidia wananchi pindi wanapotaka kufyatua tofali 200 hadi 1,000 kwa ajili ya kuongeza kibanda wasibadilishiwe gharama ya maji kutoka gharama ya maji ya nyumbani hadi gharama ya kiwanda au biashara.
Awali akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya moja kati ya wananchi kuhusu kupandishiwa gharama ya maji baada ya kufyatua tofali,Winfred Mahali,Mkuu wa kitengo cha huduma kwa wateja MAKUWASA ,amesema kuwa mteja anatakiwa kutoa taarifa kabla ya kubadili matumizi ya maji ambayo yanatofautiana na usajili wa awali, na pindi ikigundulika maji yametumika kinyume na usajili wa mteja Mamlaka itambadilisha mteja bila kumpa taarifa kwani ni kosa kubadili matumizi.
Amesema kuwa,wateja wa huduma ya maji wamegawanyika kwenye makundi matano,wateja wa majumbani, taasisi, ujenzi,biashara na viwanda na bei zake zinatofautiana kwani matumizi ya nyumbani hayafanani na matumizi katika nyumba ya biashara na kiwanda.
Ameongeza kuwa uniti Moja ya maji ni sawa na lita 1,000 za maji ambazo ni sawa na ndoo 50 za lita 20,na gharama ya maji kwa wateja wa majumbani uniti moja ni 1,500 na biashara uniti moja inauzwa shilingi 3,000.
Pia,amesema kuwa MAKUWASA kwa sasa ipo kwenye mpango wa kufunga mita za kulipia kabla ya matumizi, ambapo mteja atalipia uniti za maji anazohitaji na bei za uniti hazitabadilika ila mfumo wa ulipaji maji ndiyo utakaobadilika ambapo kwa sasa mteja anatumia ndipo analipia na mfumo mpya utamtaka mteja kulipia ndipo atumie kama ilivyo kwenye umeme wa luku.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa