Na. Lina Sanga
Kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Waziri Kindamba kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Makambako,Bw. Kenneth Haule kutumia utaratibu wa benki katika utoaji na ufuatiliaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu inayotolewa na halmashauri kupitia idara ya maendeleo ya jamii,benki ya NMB tawi la makambako wamepokea agizo hilo na wameahidi kushirikiana na halmashauri katika utekelezaji wa agizo hilo.
Mhe. Kindamba alitoa agizo hilo katika mkutano maalumu wa baraza la Madiwani la kuwasilisha mpango kazi na majibu ya menejimenti kwa ajili ya utekelezaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kuishia Juni 30,2021,lililofanyika Juni 14,2022 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Mji Makambako.
Akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa halmashauri ya Mji Makambako leo,Meneja wa benki ya NMB tawi la Makambako Bi. Olipa Hebel amesema kuwa,wapo tayari kushirikiana katika utoaji wa elimu ya matumizi ya fedha kwa wanufaika wa Mikopo hiyo,ili kuwasaidia wanufaika hao kutumia fedha hizo katika malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa muda uliopangwa.
“Sisi NMB Makambako tuna afisa ambaye amehudhuria mafunzo ya utoaji wa mikopo ya vikundi,na yupo tayari kushirikiana na halmashauri katika utoaji wa elimu ya fedha na mikopo,ili kuwajengea uwezo wanufaika wa mikopo ya asilimia kumi kupata manufaa kupitia mikopo hiyo na kurejesha kwa wakati,ili na wengine waweze kunufaika kupitia mikopo hiyo”,alisema Olipa.
Olipa amesema kuwa mbali na utoaji wa elimu ya fedha na mikopo kwa wanufaika hao,pia watashiriki katika zoezi la utoaji wa mikopo hiyo ili kurahisisha zoezi la ufuatiliaji wa madeni kwa vikundi ambavyo havijafanya marejesho kwa wakati.
Pia Olipa pamoja na Maafisa wa benki alioongozana nao walitoa elimu mbalimbali kuhusu huduma zinazotolewa na benki ya NMB,kwa wakuu wa idara na vitengo ikiwa ni pamoja na huduma ya Malipo ya kabla,Mkopo kadi na NMB mkononi.
Naye Bi. Zuena Ungele Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii katika halmashauri ya Mji Makambako, kwa niaba ya Mkurugenzi ametoa shukrani kwa Uongozi wa benki ya NMB,kwa kujitoa kushiriki katika zoezi zima la utoaji mikopo ya asilimia kumi kwa vikundi vya Wanawake ,Vijana na Watu wa wenye Ulemavu na kuahidi kushirikiana na afisa aliyeteuliwa kutoka benki hiyo bega kwa bega ili kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa.
Zaidi ya vikundi 30 vya Wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu katika halmashauri ya Mji Makambako vilivyonufaika na mkopo huo, havijafanya marejesho ya mikopo yao, hali inayokwamisha jitihada za Serikali za kuwawezesha wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kuinuka kiuchumi na kufanya mabadiliko ya kiuchumi kuanzia ngazi ya familia,jamii na Taifa kwa ujumla.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa