Na. Lina Sanga
Menejimenti ya TASAF makao makuu nchini imefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kupitia mfuko wa TASAF,katika Halmashauri ya Mji Makambako na kuwapongeza wananchi kwa kushiriki katika ujenzi wa miradi kwa kuchangia asilimia 10 na kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo hadi kukamilika pamoja na wanufaika wa TASAF katika Mtaa wa Idofi ambao walipewa Miche ya parachichi.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Usetule na Ibatu,Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF nchini, Ndg. Shandrack Mziray , amesema kuwa maeneo mengine kuchangia asilimia 10 ni changamoto lakini katika Halmashauri ya Mji Makambako ,wananchi wamejitoa kwa moyo mkubwa kuchangia na kushiriki hadi kukamilika kwa miradi hali inayoonyesha wananchi wana kiu ya maendeleo.
Aidha,amepongeza jitihada za uongozi wa Halmashauri ya Mji Makambako kwa kushirikisha wananchi kila hatua ya utekelezaji ,ufuatiliaji na usimamizi wa miradi,na kuwapa nafasi wananchi kuimiliki miradi kwa asilimia mia moja na kuondoa maswali kati yao,kwa miradi hiyo kutekelezwa kwa uwazi hali ambayo inasaidia wananchi kutambua kiasi cha fedha za utekelezaji wa miradi na kuona namna ya kuchangia ili miradi ikamilike na kubakiwa na fedha.
Pia, amewatoa hofu wananchi hao kuhusu maombi ya kutumia fedha zilizobaki baada ya miradi kukamilika na kuwaahidi kuruhusu, fedha hizo kutumika kama wananchi walivyoomba ,ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba pacha ya walimu shule ya Msingi Magomati katika Kata ya Mahongole na Uboreshaji wa miundombinu zahanati ya Ibatu katika Kata ya Kitandililo pamoja na ujenzi wa jiko la nje nyumba ya watumishi katika zahanati hiyo.
Timu ya menejimenti ya TASAF imetembelea na kukagua miradi mitatu ambayo ni ujenzi wa madarasa 6 na matundu 12 ya vyoo shule ya msingi Magomati,Kijiji cha Usetule,Ujenzi wa nyumba pacha ya watumishi zahanati ya Ibatu na mradi wa parachichi kwa wanufaika wa TASAF.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa