Na. Lina Sanga
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi(sekta ya mifugo) inatarajia kutengeneza mfumo wa kielekitroniki utakaotumika kuwasajili Maafisa Ugani wote pamoja na wafugaji,ili kubaini utendaji kazi wa maafisa hao na idadi ya wafugaji waliopata huduma kwa siku kwa lengo la kuongeza uwajibikaji katika sekta hiyo.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi(sekta ya mifugo), Mhe. Tixon Nzunda katika kikao cha ufunguzi wa mafunzo rejea, kwa maafisa ugani wa Mikoa ya nyanda za juu kusini,yanayoanza leo katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Makambako na kuhitimishwa kesho novemba 18,2022.
Mhe. Nzunda amesema kuwa huduma za ugani ni pamoja na uwajibikaji na kubainisha kuwa kuna baadhi ya Maafisa ugani wanalipwa mishahara kwa kufanya kazi kidogo,kazi ambazo haziwezi kupimwa na zina matokeo kidogo hivyo kupitia mfumo huo wa kielekitroniki utasaidia kuimarisha mfumo wa huduma za ugavi na kuongeza uwajibikaji wa Maafisa ugani wote.
Ameongeza kuwa, juhudi za kuishawishi Serikali kuongeza idadi ya Maafisa Ugani nchini ili kuendana na mpango wa mabadiliko wa Sekta ya Mifugo kwa mwaka 2022/2023 zinaendelea,ili wafugaji wote wafikiwe na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa Maafisa ugani katika ngazi ya msingi ambapo kwa sasa idadi ya Maafisa ugani ni chini ya asilimia 12.
Pia,amebainisha kuwa jumla ya mashamba darasa 100 ya malisho yataanzishwa nchini ili kuwafundisha wafugaji kuwa na mashamba ya malisho,kwa ajili ya mifugo yao na kuachana na tabia ya kuhamahama kutafuta malisho.
Ameongeza kuwa,ili kuimarisha sekta hiyo Serikali imeamua kujenga minada 45 yenye mizani na kutengenza mfumo wa kielekitroniki ili ng’ombe kutoka Tanzania anunuliwe na mtu yeyote kote duniani,kwani kupitia mfumo huo watu wote kutoka nchi mbalimbali wataweza kuwaona ng’ombe wanapoingia kwenye mnada,wanapopigwa picha na kuingizwa kwenye mfumo ambao mtu yeyote anaweza kuusoma.
Ili kuongeza uwajibikaji wenye tija Wizara ya Mifugo na Uvuvi(sekta ya mifugo) kwa mwaka wa fedha 2022/2023,inatarajia kununua jumla ya pikipiki 1,200 ambazo zitaelekezwa kwenye mikoa inayotekeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyama na magari 13.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa