Na. Lina Sanga
Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Mhe. Anthony Mtaka leo amefanya uzinduzi wa mradi wa upandaji wa miti ya parachichi kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini -TASAF katika Kata ya Mlowa,iliyopo Halmashauri ya Mji Makambako ikiwa ni sehemu ya kampeni ya Mkoa wa Njombe kutokomeza umasikini.
Mhe. Mtaka amesema kuwa jumla ya miche 20,000 ya parachichi yenye thamani ya mil. 100 imetolewa na Wizara ya Kilimo,hivyo Mkoa wa Njombe umeona ni vema miche hiyo itolewe kwa kaya masikini zinazonufaika na TASAF ili kuwawezesha wanufaika hao kuongeza pato la familia kwa kuuza matunda ya parachichi baada ya miaka mitatu na baada ya miaka mitano wanufaika hao wajitegemee badala ya kuitegemea TASAF maisha yao yote kwani ipo siku TASAF haitakuwepo.
Kabla ya kufanya uzinduzi huo Mhe. Mtaka amewataka wananchi wote kuwahimiza watoto wao kusoma kwani Serikali imekopa Bil. 300 ili kujenga madarasa na haitakuwa tayari kuendelea kukopa Bil. 400 kwa ajili ya kuwapa wazee ambao walikataa shule na kuendekeza ulevi.
Ametoa rai kwa wanufaika wote wa TASAF kuupokea mradi huo wa upandaji wa parachichi na kumuagiza Mratibu wa TASAF katika Halmashauri ya Mji Makambako kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kila mnufaika wa TASAF kwa kushirikiana na Maafisa kilimo,Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji na kwa mnufaika ambaye miche itakufa aondolewe kwenye mpango wa TASAF kwani atakuwa amefanya makusudi kuuhujumu mradi.
Mkoa wa Njombe una jumla ya wanufaika wa TASAF 25,000 na Halmashauri ya Mji Makambako ina jumla ya wanufaika wa Mpango wa TASAF1,825 ambao wanatarajiwa kupewa miche 10 kwa kila kaya na upandaji wa miche hiyo utafanyika februari 1,2023 katika sherehe ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa