Na. Lina Sanga
Njombe
Mikataba yenye thamani zaidi ya Bil. 22 ya ujenzi wa barabara Mkoa wa Njombe imesainiwa leo,ikiwa ni sehemu ya pili baada ya mikataba hiyo kusainiwa kwa awamu ya kwanza Mkoani Dodoma Agosti 14, mwaka huu mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) Mkoa wa Njombe,Mhandisi Gerald Matindi katika kikao cha utiaji saini mikataba ya matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja, awamu ya pili kwa asilimia 40,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Mhandisi Matindi,amesema kuwa lengo la kusaini mikataba hiyo kwa awamu ya pili katika ngazi ya Mkoa, baada ya ngazi ya Taifa ni kutoa umiliki wa miradi hiyo kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe ili waweze kupokea miradi ambayo toka miaka mitatu iliyopita imeongezeka kwa asilimia 37.
Amesema kuwa,kupitia mikataba hiyo TARURA kwa mwaka huu wa fedha, itafanikiwa kukamilisha matengenezo ya barabara zenye jumla ya kilomita 1,175.7 ambazo ni kilomita 8.9 za barabara zenye kiwango cha lami, kilomita 735.99 barabara zenye kiwango cha changarawe na matengenezo ya kawaida kilomita 430 pamoja na ujenzi wa madaraja 41.
Aidha,amebainisha kuwa Mikataba 22 iliyosainiwa leo ni sehemu ya Mikataba 32, yenye asilimia 60 ya fedha zote zilitakiwa kutolewa katika mwaka huu wa fedha ambayo ilisainiwa Agosti 14,mwaka huu Mkoani Dodoma.
Halmashauri ya Mji Makambako imepata jumla ya Bil 2.8 ambapo bil. 1 ni fedha za tozo ya mafuta zitazotumika katika matengenezo ya barabara ya Lumumba na barabara ya Madunda kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1 zilizopo Kata ya Mwembetogwa na matengenezo kwa kiwango cha changarawe na kifusi barabara ya mbugani na usetule yenye kilomita 12 na barabara ya Kitandililo na Wangama yenye kilomita 13.
Bil. 1 ya maendeleo ya jimbo itatumika katika matengenezo ya barabara ya Ds na A-one kwa kiwango cha lami na jumla ya mil. 831 zitatumika katika matengenezo ya kawaida ya kilomita 166 za barabara na ujenzi wa madaraja 4.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa