Na. Lina Sanga
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi(sekta ya mifugo), Mhe. Tixon Nzunda ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwenye vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu kupitia Idara ya maendeleo ya jamii inawafikia vijana wanaojishughulisha na ufugaji kupitia program iliyoanzishwa na Serikali ya kuwawezesha vijana kuunda vikundi vya ufugaji.
Mhe. Nzunda ametoa kauli hiyo leo katika kikao cha ufunguzi wa mafunzo rejea kwa Maafisa ugani wa Mikoa ya nyanda za juu kusini,yanayofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Makambako.
Amesema kuwa, kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 Serikali imeanzisha vituo nane vya unenepeshaji ng’ombe ambavyo vijana wasomi waliosomea masuala ya sekta ya mifugo kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada wameunda vikundi vyenye watu 30,ambavyo vinajishughulisha na uwekezaji wa kunenepesha mifugo na kila kikundi kimepata ng’ombe 300 na kila kijana amepewa ng’ombe 10 awahudumie.
Ameongeza kuwa jukumu la Serikali na Halmashauri katika program hiyo ni kuwajengea mazingira wezeshi vijana ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha,kujenga mazizi,kujenga majosho,kuandaa malisho,fedha za kuandaa malisho pamoja na vifaa vinavyotumika kuandaa malisho kwa mtindo wa kuwakopesha,ambapo baada ya fedha kupatikana faida itayopatikana itaingizwa kwenye akaunti ya kikundi kama faida mara nne kwa mwaka na baadaye vikundi hivyo vitasajiliwa kama vikundi vya ushirika.
“Baada ya kusajiliwa kama kikundi cha ushirika watapatiwa maeneo ya ufugaji au Halmashauri moja moja itawatafutia maeneo ya uwekezaji kupitia mtaji wao,kwa ajili ya kuanzisha vituo vya unenepeshaji wa mifugo na kuwaunganisha na taasisi za fedha ili waweze kukopesheka kwani watakuwa tayari wanatambulika kwa kufanya hivi hawa watakuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya ufugaji wenye tija”,alisema Mhe. Nzunda.
Ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya malisho na kuwagawia wafugaji,ili kuwawezesha wafugaji kuwa na uhakika na malisho ya mifugo yao na kufuga mifugo kisasa.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa