Na. Lina Sanga
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Waziri Kindamba amewaagiza waajiri wa taasisi mbalimbali mkoani hapa kufanya vikao mara kwa mara na wafanyakazi kwa kushirikiana na Vyama vya wafanyakazi ili kutatua kero za wafanyakazi na kujenga umoja sehemu za kazi.
Mhe. Kindamba ametoa agizo hilo baada ya kusomwa kwa risala iliyobeba changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa serikali na taasisi binafsi mkoani hapa, katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika leo Kimkoa katika viwanja vya polisi katika Halmashauri ya Mji Makambako na kuhudhuriwa na wafanyakazi wa sekta mbalimbali.
Amesema kuwa tabia ya baadhi ya waajiri kutofanya mabaraza ya wafanyakazi ambayo yanatakiwa kufanyika mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya kujadili na kutatua kero na changamoto mbalimbali za watumishi,kuhakikisha wanafanya mabaraza hayo na watambue kuwa kufanyika kwa mabaraza ya wafanyakazi ni agizo ambalo kwa mara ya kwanza lilitolewa mwaka 1970 chini ya utawala wa Rais wa awamu ya kwanza wa Tanzania,hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Kuhusu madeni ya watumishi Mhe. Kindamba amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 mkoa wa Njombe umelipa madeni ya watumishi jumla ya shilingi Mil.370 ikiwa ni malimbikizo ya mishahara,madai ya uhamisho na matibabu na serikali inaendelea kulipa madeni hayo kila mara baada ya uhakiki kukamilika.
Pia Mhe. Kindamba amewaasa waajiri kulipa stahiki mbalimbali za watumishi wa sekta ya afya ikiwa ni pamoja na Malipo ya masaa ya ziada na kuitwa kazini,kwani ni haki yao kwa mujibu ya sheria hivyo kila anayestahili kulipwa alipwe.
Kuhusu uhaba wa watumishi na vitendea kazi, Mhe. Kindamba amesema kuwa Serikali inaendelea kuongeza watumishi ili waendelee kutoa huduma,na hivi sasa ajira mpya katika kada ya afya 7,612 zimetangazwa pamoja na kada ya elimu na mkoa wa Njombe pia unatarajia kupokea watumishi wapya,na kuhusu uhaba wa watumishi maeneo yenye mazingira magumu,Serikali inaendelea kuongeza watumishi maeneo yenye mazingira magumu ikiwemo ukanda wa ziwa nyasa kupitia utaratibu wa msawazo ndani ya mkoa kila robo Mwaka.
Aidha,Kuhusu watendaji wasio waaminifu kunyofoa nyaraka za ofisi ili kuzuia mtumishi asipate stahiki zake,Mhe. Kindamba amewatahadhalisha watumishi au watendaji wenye tabia hiyo kuacha mara moja,na kuagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi wa malalamiko hayo na kuwachukulia hatua za kinidhamu,kwani fedha anazolipwa mtumishi hazitoki mifukoni mwao hivyo watumishi hao waache roho mbaya.
Pia ametoa wito kwa waajiri kuwaruhusu watumishi kujiunga na vyama vya wafanyakazi na kuhakikisha wanafikisha michango yao kwenye mifuko ya hifadhi za jamii kama NSSF na PSSSF,ili kuwawezesha watumishi kupata mafao yao pindi wanapostaafu na kuvitaka vyama vya wafanyakazi kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Mwisho amewataka watumishi na wananchi wote mkoani Njombe kuchukua tahadhali dhidi ya maambukizi ya UKIMWI kwani takwimu za Maambukizi zipo juu sana ,lakini pia kila mwananchi ahakikishe anapata chanjo ya Uviko 19 ili kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa Korona, pamoja na kujiandaa kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi Agosti 23,2022.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa