Na. Lina Sanga
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda amezitaka kamati zinazohusika na michakato ya mikopo ya vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri katika Halmashauri ya Mji Makambako kutokuwa kikwazo cha kuwawezesha wajasiriamali kupata mikopo inayoendana na miradi yao ili mikopo hiyo iwe chanzo cha utajiri katika Mji wa Makambako na kuongeza ajira.
Mhe. Sweda ametoa wito huo leo katika hafla ya utoaji wa mikopo awamu ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/2025 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri,ambapo jumla ya mil. 350.8 zimetolewa kwa vikundi 11 vya wanawake, vikundi 17 vya vijana na watu wenye ulemavu 2.
Amesema,ili kutimiza lengo la Serikali kuwainua wananchi kiuchumi kamati za mikopo zifanye majadiliano na vikundi vilivyoomba mikopo ili kujifunza kabla ya kupunguza kiasi cha mkopo na kuathiri utekelezaji wa miradi na kuvitaka vikundi vilivyopata mikopo kufanya kazi na kuhakikisha vinafanikiwa kupitia mikopo hiyo, kwani Serikali ya awamu ya sita imetengeneza mazingira rafiki ya wananchi kujiingizia kipato kwa amani.
Bi. Agatha Mhaiki,Katibu Tawala wilaya ya Njombe amewataka wanufaika wa mikopo kutumia fedha hizo vizuri ili kutimiza malengo waliyojiwekea badala ya kufanyia starehe.
Nickson Mlula,Maria Mdoma na Stesha Gawasike ni moja kati ya wanufaika wa mikopo hiyo kwa awamu ya pili kupitia vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu ambapo kwa Pamoja wameishukuru Serikali kwa kutoa mikopo rafiki isiyo kuwa na riba ili kuwawezesha wananchi kuinuka kiuchumi na kuahidi kurejesha kwa wakati.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa