Na. Lina Sanga
Mil. 583 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule Mpya ya Sekondari ya Kata ya Mjimwema, ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya Makambako sekondari.
Akitoa taarifa hiyo leo Afisa elimu wa divisheni ya elimu sekondari katika Halmashauri ya Mji Makambako, Mwl. Aderick Nombo amesema kuwa, shule hiyo ya Kata ya Mjimwema itajengwa katika Mtaa wa Igangidung'u katika Kata ya Kivavi, kutokana na Kata ya Mjimwema kukosa eneo la ujenzi wa shule.
Amesema kuwa, awali Kata ya Mjimwema waliazimia kujenga shule hiyo katika eneo la shule ya Msingi Makambako, lakini imeshindikana kutokana na eneo hilo kutokidhi vigezo.
Ametoa wito kwa wananchi wa Kata ya Mjimwema kujitoa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo kwani licha ya kujengwa kwenye Kata ya Kivavi, wana umiliki wa shule na inatambulika kama shule ya sekondari ya Kata ya Mjimwema na siyo Kivavi, lakini pia wananchi wa Kata ya Kivavi watanufaika kupitia shule hiyo kwa kuwasomesha watoto wao hivyo wananchi wa Kata zote mbili wana wajibu wa kushiriki ujenzi wa shule hiyo.
Mhe. Nolasco Mlowe, diwani wa Kata ya Mjimwema ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo, na kuahidi kushiriki kusimamia mradi huo hadi utakapokamilika kwa kushirikiana na wananchi wa Kata yote ya Mjimwema.
Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Igangidung'u, Nasibu Mabiki ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule hiyo katika Mtaa huo na kuahidi kushirikiana bega kwa bega na viongozi wa Kata ya Mjimwema na wananchi kwa ujumla hadi mradi utakapokamilika , kwani maendeleo hayana Mtaa wala Kata wananchi wa Kata na Mitaa yote watanufaika kupitia shule hiyo.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa