Na. Lina Sanga
Kamati ya ujenzi ya Zahanati ya mtulingala iliyopo Kijiji cha Mtulingala Kata ya Kitandililo katika Halmashauri ya Mji Makambako, imepongezwa na Kamati ya Fedha na Uongozi kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa Zahanati hiyo kwa viwango vinavyokubalika.
Pongezi hizo zimetolewa leo katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Mji Makambako,mara baada ya ukaguzi wa mradi huo ambao kwa sasa upo hatua ya ukamilishaji.
Aidha,Mhe. Rosemary Lwiva,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako amepongeza Serikali ya Kijiji na wananchi kwa ujumla kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Zahanati hiyo kwa kuchangia jumla ya Mil. 21.3 hali inayodhihirisha uhitaji wa Zahanati katika Kijiji hicho.
Pia,amewapongeza wananchi kwa kuendelea kujitoa kufanya shughuli mbalimbali katika eneo la mradi kama uchimbaji na ujenzi wa shimo la choo,ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kutaka kila Kijiji kuwa na Zahanati ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi.
Ametoa rai kwa Mkurugenzi na Menejimenti kuona namna ya kuchangia shughuli zilizobaki,ili Zahanati hiyo ianze kufanya kazi ili kuwapunguzia mwendo wananchi wa kufuata huduma za afya na na kuwapa nguvu ya kuendelea kushiriki kwenye miradi mingine zaidi.
Mzee Onesmo Ndumbula,Mkazi wa Kijiji cha Mtulingala kwa niaba ya wananchi wa Kijiji hicho, ameishukuru Kamati ya Fedha na Uongozi kwa kutambua kazi kubwa iliyofanywa na wananchi wa Kijiji hicho ya kujenga Zahanati na kwa pongezi hizo wamefarijika na imewatia moyo wa kuendelea na kazi.
Naye Mhe. Imani Fute,diwani wa Kata ya Kitandililo ametoa rai kwa Serikali kuwa,mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa choo na kichomea taka, huduma za awali kama kliniki za kina mama na watoto zianze kutolewa ili kuwapunguzia mwendo wananchi kufuata huduma hizo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako,Eliud Mwakibombaki amewatoa hofu wananchi wa Kijiji hicho na kuwahakikishia kuwa kwa kushirikiana na Kamati ya Fedha na Uongozi,kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 wataona namna ya kupata fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa Zahanati hiyo ili ianze kutoa huduma mara moja.
Mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mtulingala uliibuliwa na wananchi na kwa sasa upo katika hatua ya ukamilishaji, ukiwa umegharimu jumla ya Mil. 89 ikiwa ni fedha Kutoka Serikali Kuu, Mchango wa Mbunge wa jimbo la Makambako, wananchi, wadau wa maendeleo na Halmashauri kupitia mapato ya ndani.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa