Na. Lina Sanga
Miradi sita yenye thamani ya shilingi bil. 4.7 iliyopitiwa na mwenge wa uhuru katika halmashauri ya Mji Makambako jana, imekaguliwa, kutembelewa na kuzinduliwa kwa kuzingatia ubora wa mradi na thamani ya fedha zilizotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Madarasa matatu na ofisi moja kwa fedha za tozo za miamala ya simu katika shule ya sekondari Mlumbe iliyopo katika kata ya Lyamkena,ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami mtaa wa Soko la Mbao katika Kata ya Mjimwema,Mradi wa vijana wa kikundi cha Juhudi ambao ni wanufaika wa mkopo wa asilimia kumi inayotolewa na halmashauri katika mtaa wa Mlando,Nyumba ya mhanga wa maafa ya upepo mkali mtaa wa Lupila katika Kata ya Kitisi,Mradi wa kunenepesha ng’ombe,mbuzi na kondoo mtaa wa Kihanga katika kata ya Mlowa na Ujenzi wa jengo la maabara katika kituo cha Afya Kitandililo.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa,ndg. Sahili Geraruma amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo lakini pia juhudi za wananchi katika kuchangia maendeleo kwenye maeneo yao na kuwataka Watendaji wa Serikali kusimamia miradi hiyo kwa ukaribu na kurekebisha kasoro ndogondogo katika baadhi ya miradi iliyokaguliwa na Mwenge.
Aidha Geraruma amewataka vijana kuanzia miaka 18 kuunda vikundi kwa ajili ya kupata mikopo ya ailimia kumi inayotolewa na halmashauri na kuzifanyia kazi ili kukuza uchumi wa taifa, badala ya kujihusisha na vitendo viovu kama kuvuta bangi na matumizi ya dawa za kulevya,pia wanawake na watu wenye ulemavu waunde vikundi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri zote Nchini.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Kitisi baada ya kuzindua nyumba ya Bi. Tumwihuhage Kihwele iliyojengwa na serikali baada ya bibi huyo kukosa makazi kutokana na nyumba aliyokua akiishi kubomolewa na Upepo mkali, Geraruma amesema kuwa falsafa ya Mwenge ni kuleta tumaini mahali pasipo na matumaini,hivyo Tumwihuhage amepata tumaini jipya kupitia ujenzi wa nyumba hiyo pamoja na kitukuu chake.
Bi. Tumwihuhage ambaye ana umri zaidi ya miaka sitini ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kumjengea nyumba hiyo,na kuwa hakutegemea kumiliki nyumba hiyo pamoja na kitukuu chake kwani hana msaada wowote baada ya watoto wake wote kufariki.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa