Na. Lina Sanga
Ludewa
Mwenge wa Uhuru 2023 umepokelewa leo katika Mkoa wa Njombe kutoka Mkoa wa Ruvuma, na utakimbizwa katika Halmashauri 6 za Mkoa huo kwa umbali wa 517KM na kutembelea,kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo 45 yenye thamani ya Bil. 346.5.
Akisoma taarifa ya Mwenge wa Uhuru mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2023,Ndg. Abdalla Shaibu Kaim ,Katibu Tawala Mkoa wa Njombe,Bi. Judica Omari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe amesema kuwa,Mkoa huo unaendelea kutekeleza ujumbe mkuu wa Mwenge wa Uhuru na jumbe za kudumu kwa kusimamia utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na lishe,mapambano dhidi ya UKIMWI,mapambano dhidi ya dawa za kulevya,malaria, mapambano dhidi ya rushwa na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.
Amesema kwa mwaka 2022,Mkoa wa Njombe umefanikiwa kupanda jumla ya miti Mil. 30 ya mbao na matunda sawa na asilimia 341 na kwa 2023 katika miezi kadhaa jumla ya miti Mil. 26.5 sawa na asilimia 327 imepandwa na uhamasishaji wa upandaji unaendelea hadi msimu wa mvua utakapo malizika ili kutunza vyanzo vya maji na mazingira.
Amebainisha kuwa,hadi sasa Mkoa huo una jumla ya vyanzo vya maji 3,377 na vyanzo vya maji 1,730 sawa na asilimia 50.4 vimehifadhiwa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka uzio.
Aidha ,amesema kuwa kwa upande wa lishe bora jitihada mbalimbali zimeendelea kufanyika kwa kutoa elimu ya lishe kwa jamii na kuwahamasisha kula chakula bora,ili kutokomeza udumavu ambapo kwa takwimu za mwaka 2018 udumavu ulikua asilimia 53 na kwa kipindi cha mwaka 2022 udumavu umeshuka hadi asilimia 50.
Katika mapambano dhidi ya Malaria,kiwango cha Maambukizi ya ugonjwa huo ni asilimia 1.9 na jitihada mbalimbali za kutokomeza ugonjwa huo zinaendelea kufanyika kwa kutoa elimu na kinga dhidi ya malaria pamoja na ugawaji wa vyandarua kwa watoto wadogo na kina mama wajawazito.
Pia,katika mapambano dhidi ya ukatili, Bi. Judica amebainisha kuwa jumla ya mashauri 479 yaliripotiwa katika ofisi za Ustawi wa jamii na madawati ya jinsia,kati ya mashauri hayo migogoro ya ndoa ni 223, utekelezaji wa watoto 156,ukatili wa kimwili 22,ulawiti 14 na ubakaji 15 na mashauri yote yameshughulikiws kwa mujibu wa kanuni na sheria.
Ameongeza kuwa,Mkoa wa Njombe unakabiliwa na tatizo dogo la matumizi ya bangi ,kwa vijana wenye umri kati ya miaka 17 hadi 28 na jeshi la polisi linaendelea kudhibiti matumizi ya bangi.
Kuhusu Mapambano dhidi ys rushwa jumla ya kesi 8 zilifunguliwa katika kipindi cha mwezi julai 2022,kesi 3 zilishinda,kesi 1 ilishindwa na kesi 4 zinaendelea na mapambano dhidi ya UKIMWI yamepungua kutoks asilimia 14 hadi asilimia 11.4 na Mkoa wa Njombe una jumla ya watu 65,000 wanaoishi na Maambukizi.
Mwenge wa Uhuru utazunguka katika Halmashauri 6 za Mkoa wa Njombe kwa siku 6 na Aprili 30,utakimbizwa katika Halmashauri ya Mji Makambako na kukabidhiwa Mei mosi,2023 Mkoa wa Iringa.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa