Na. Lina Sanga
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Makambako, Bw. Kenneth Haule amekiri kutofurahishwa na tabia ya baadhi ya wamiliki wa stoo za mazao, wanaoendeleza mgomo wa kuhamisha stoo za mazao zilizopo kwenye makazi ya watu,licha ya kupewa elimu juu ya utekelezaji wa zoezi hilo lililoanza zaidi ya miaka mitano na kuwazomea maafisa wa Serikali wanaosimamia utekelezaji wa zoezi hilo ili kukwamisha zoezi.
Haule , amesema hayo leo katika kikao na baadhi ya viongozi wa wafanyabiashara wa mazao, waliofika kutoa maoni na mapendekezo ya baadhi ya wafanyabiashara ambao bado hawajahamia katika soko la mazao la Kiumba,kwa madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuomba muda zaidi wa kukamilisha ujenzi wa vizimba baada ya nyongeza ya muda kuisha na ujenzi kutoendelea kulingana na makubaliano ya awali.
Amesema kuwa, baadhi ya wafanyabiashara ambao wamegomea zoezi la kuhamisha stoo za mazao na kuanzisha maandamano yasiyo rasmi wala tija yakiongozwa na wanawake,si kigezo cha kutohama,kwa mfanyabiashara atayekutwa akifanya biashara ya mazao,kushusha au kupakia mazao eneo lisilo rasmi atalipishwa faini isiyopungua laki tano pamoja na mwenye gari na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.
Ametoa rai kwa wafanyabiashara hao kutii sheria bila shuruti kwani sheria haichagui mfanyabiashara mkubwa au mjasiriamali mdogo, na Halmashauri haitoi muda mwingine tena wa utekelezaji wa zoezi hilo kwa sasa kwani hoja zinazotolewa hazina mashiko.
Bi. Amina Kassim,Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji Makambako ametoa rai kwa wafanyabiashara kuzingatia mikataba yao, waliyosaini ya ujenzi wa maghala na vizimba katika soko la mazao la Kiumba na kutofuata mkumbo katika kukamilisha ujenzi na kuhama,kwani Mkataba ulijazwa na Mtu mmoja sio kundi hivyo Halmashauri itashughulika na mtu mmoja mmoja na sio kundi la watu.
Makambako Town Council
Anuani ya Posta: P.O.BOX 405 Makambako
Simu ya mezani: 026-2730044
Simu ya Kiganjani: 0785635383
Barua pepe: td@makambakotc.go.tz
Haki miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Makambako. Haki zote zimehifadhiwa